Moduli 3, Wadudu na udhibiti wa magonjwa (revised)

Page 1

Mkulima Mbunifu Moduli namba 3

WADUDU NA UDHIBITI WA MAGONJWA Kilimo hai ni aiana ya kilimo ambacho kinalenga kuleta ukombozi na uangalifu mkubwa katika kuondokana na matumizi ya pembejeo hatari. Kwa kawaida hujumuisha hathari kubwa: Uchafuzi na madhara ya muda mrefu wa mazingira, vyanzo vya maji, na kuathiri wakulima na familia zao. Hivyo kilimo hai kinalenga kutekeleza njia ambazo haziruhusu kuwepo kwa kiasi kikubwa cha wadudu waharibifu. Kinajaribu kuepuka matumizi ya moja kwa moja ya njia za udhibiti zenye madhara.

Wakati wote: Hatua za kujikinga!

Hatu za moja kwa moja (Uk 2-4) Kuna uwiano wa ufanisi wa dawa za kuulia wadudu na ukungu kwenye mimiea na madini yanayoweza kutumika kwenye kilimo hai. Siyo yote ambayo hayana madhara isipokuwa kopa, kwa kawaida viini vyake huyeyuka haraka kuliko kemikali nyingine za kawaida.

Lima kwa mzunguko mara kwa mara. Hii ni moja ya mbinu yanye mafanikio makubwa katika kilimo hai, kudhibiti magonjwa na magugu yanayofungamana na jamii fulani ya mazao. Kuwezesha rutuba kwenye udongo. Tumia mbolea za asili kama vile mboji na samadi kusaidia kuimarisha rutuba kwenye udongo na afya ya mimea.

Baadhi ya mimea inayotumika kama dawa na dawa za kunyunyiza kwa ajili ya udhibiti wa wadudu na magonjwa, zinaweza kutengenezwa kwa urahisi na wakulima wadogo. Tafadghali soma pia moduli ya Mkulima Mbunifu “Madawa maalumu ya asili” Kuepukana na magonjwa ya mbegu, mbegu zinaweza kutibiwa kwa maji ya moto.

Chagua aina ya mazao yanayokabiliana na magonjwa. Hizihazihitaji nguvu ya ziada kuzilinda. Dumisha wadudu wa asili. Kwa kawaida hawa hudhibiti wadudu wa haribifu kwa ufanisi mkubwa. Fahamu kuwa kwa kawaida viuatilifu huua wadudu rafiki pamoja na ukungu.

Udhibiti wa wadudu: Wadudu wa asili ni rafiki kwa mkulima Kwenye mazingira ya asili, utawakuta siyo tu wadudu waharibifu, lakini pia viumbe hai wengi wenye faida ambao humsaidia mkulima kudhibiti wadudu waharibifu. Ni vigumu sana kwa aina fulani ya kizazi cha wadudu waharibifu kuongezeka endapo kuna aina nyingine ya wadudu wanaowala.

Nyigu wadogo hutagia mayai yao juu ya wadudu wengine. Mfano kwenye mdomo wa katapila, ambao huanza kuharibu kabichi ambazo ungeanza kuuza muda mfupi tu ujao. Viluwiluwi wa nyingu hujilisha kutokana na wadudu, viluwiluwi, kuwaua, na hivyo kusaidia kuokoa kabichi zako ambazo pengine hata usingegundua lolote.

Mfano Bungo jike, na viluwiluwi wao kwa kiasi kikubwa huliwa na vidukari. Buibui kwa kiasi kikubwa hukamata minyoo na wadudu wengineo.

Pia kuna minyoo, fangasi, na iana nyingine ya wadudu wadogo wadogo ambao wanaweza kuwadhuru na kuwaua wadudu waharibifu, kwa mfano inzi weupe, katapila, bungo au panzi.

Mayai

Viluwiluwi walioanguliwa

Kiluwiluwi mkubwa

Pupa

Unaweza kufanya nini kuweka uwiano wa kiasili • Chagua aina ya zao ambalo halidhaniwi kushambuliwa sanana wadudu na magonjwa. • Tunza wadudu rafiki katika shamba lako. Si lazima kuwafahamu wote, lakini ni vizuri kufahamu kuwa wapo shambani mwako na namna ya kuwatunza. • Uzio na miti si tu kuwa hutoa malisho kwa mifugo, nguzo na kuni, lakini pia hutoa makazi kwa wadudu wenye rafiki kwa mkulima. Nyasi, mimea inayochanua, uwanda ambao haujanyunyizwa dawa, na sehemu yenye msitu ndio maeneo ambayo wadudu rafiki wanaweza kupatikana na kuendelezwa kwa kiasi kikubwa.

Bungo mkubwa

Watu walio wengi hawawezi kutambua aina nyingi za wadudu na hatua zao za ukuaji: mayai, kiluwiluwi, pupa, na mdudu kamili. Hapa unaweza kuona hatua mbalimbali za ukuaji wa bungo.

Tumia dawa za kuulia wadudu kwa busara Hii ifanyike pale tu ambapo kuna ulazima wa kufanya hivyo. Kwa nini: Sehemu ambapo dawa za kuulia wadudu zinatumika mara kwa mara na aina moja ya dawa kutumika kwa muda mrefu, kwa kawaida wadudu hujenga upinzani na dawa hiyo kuwa haina nguvu-na wadudu kuendelea kuishi. Aina nyingi ya dawa za kuulia wadudu pia zina madhara kwa wadudu wenye faida kwa mkulima. Lakini baadhi huwa na madhara kidogo kuliko nyingine. Ni busara kujaribu kujielimisha kuhusu aina inayopatikana na kununua ambayo ina madhara kidogo endapo kuna uwezekano wa kuchagua.


Madawa hai (Bio-pesticide)

Dawa hai zinaweza kutumika kudhibiti wadudu wanaojilisha kwenye mimea. Dawa hizi hutokana na bakteria wanaokuwa kwenye udongo ambao huzalisha aina fulani ya sumu inayoua. Unaweza pia kupata aina hizi za dawa za asili kutoka katika maduka yanayouza pembejeo. Dawa hizi unaweza kuzipata zikiwa kwenye majina kama: Thuricide, Dipel, Javelin, na Xentari. Faida ya kutumia aina hii ya viuatilifu ni za gharama ndogo,rahisi kutumia, na zina ufanisi wa hali ya juu. Hakuna madhara yanayosababishwa na dawa hizi, iwe kwa binadamu au kiumbe hai chochote mbali na wadudu waharifu.

Namna ya kutumia 1. 1. Tumia wakati viluwiluwi wakiwa bado wadogo. Viuatilifu hivi vya asili vinafanya kazi vizuri zaidi viluwiluwi wanapokuwa wadogo (Mf. Katapila) 2. Viuatilifu hai vinakuwa na ufanisi zaidi kwenye maji yenye asidi. Ongeza vijiko vichache vya vinegar kwenye galoni (lita 4) za maji kabla ya kuongeza kiasi cha dawa hai. 3. Nyunyiza wakati wa jioni wakati ambao jua limeshatua. Viuatilifu hai hufanya vizuri zaidi kwenye hali joto iliyopoa na hubaki kwenye majani kwa muda mrefu zaidi. 4. Nyunyiza kwa umakini kufunika sehemu yote ya juu ya mmea.

Diatomite siyo dawa ya kemikali

-Kwa pipa kubwa tumia kilo 3 za diatomite kwa kila tani moja ya nafaka.

Diatomite ni mchanganyiko wa viumbe hai vilivyokufa, pamoja na magugu maji. Hizi zimerundikana milioni kwa mabilioni chini ya maziwa na bahari duniani kote. Kaka lake lina ncha kali sana na ni gumu, lakini umbo lake ni dogo sana linaloweza kuonekana kwa kutumia darubini. Miamba ya Diatomite inaposagwa hutokea unga mweupe. Ni dawa ya kuulia wadudu iliyogunduliwa yapataa miaka 40 iliyopita. Mdudu anapogusana na diatomite chembechembe kali zilizoko ndani yake zinamjeruhi mdudu na kupoteza maji mwilini. Kwa kuwa pia Diatomite hufyonza maji hufanya mdudu kupoteza maji haraka na kufa. Diatomite inafanya kazi kiyabisi na siyo kikemikali. Hakuna njia yoyote ambayo mdudu anaweza kujikinga, au kujenga uwezo wa kukabiliana na Diatomite.

Tumia kudhibiti vimelea kwa mifugo

Haina madhara, ni salama

Madini ya kuulia wadudu: Diatomite Tumia kuhifadhia mazao Diatomite inaua fukusi na aina nyingine ya wadudu wanaoharibu nafaka na maharage yanapohifadhiwa. Diatomite siyo sumu, ila nafaka na maharage ni lazima vioshwe kabla ya kupika. Namna ya kutumia: -Kuhifadhia nafaka au maharage tumia gramu 500 (1/2 kg) ya diatomite kwa kila gunia moja (mahindi, mchele, ngano, mtama, n.k) changanya kwa kutumia beleshi.

Vimelea wanje: Kuku: Dhidi ya minyoo na kupe walaini, wanyunyizie vumbe la diatomite mara kwa mara, na ongeza kwenye udongo sehemu ambayo kuku huchezea/huoga kwenye vumbi mara kwa mara. Ng’ombe, nguruwe, mbuzi, sungura, mbwa, n.k: Kudhibiti kupe, viroboto, chawa, utitiri, paka wanyama wako vumbi la diatomite mara kwa mara kwenye ngozi. Unaweza pia kuweka kwenye malazi yao.

Vimelea wa ndani: Diatomite inaweza kuchanganywa na chakula cha mifugo. • Ng’ombe/farasi: 30-60g kwa siku • Kondoo/mbuzi: 15g kwa siku • Kuku/aina nyingine za ndege: 2% ya uzito wa chakula kitakacholishwa (mf. 10kg za chakula inachanganywa na 200g za diatomite) Ufanisi kwa vimelea wa ndani hauko wazi sana. Diatomite inaweza kusaidia madhara yasiyo makubwa. Kwa madhara makubwa na vimelea hatari (mf. Ruba wa ini) inahitaji tiba kamili kutoka kwa mtaalamu wa mifugo.

Tumia kukinga mazao Diatomite inaweza kutumika katika kudhibiti vidukari, utitiri, katapila, fukusi, panzi, sisimizi, Sota, konokono na wengineo. Matumizi: Kwa matumizi ya sehemu kavu ya diatomite, tumia tambara. Nyunyiza moja kwa moja kwenye mdudu. Kudhibiti sota na konokono, weka diatomite kwenye shina mmea. Sota wanapotaka kula mmea wanakumbana na unga wa diatomite na kufa. Ni vizuri kutumia Diatomite wakati ambapo kuna unyevu au baada ya mvua kidogo kunyesha. Inatakiwa kuweka tena baada ya mvua.

Kwa sababu ya chembechembe za diatomite, chembechembe hizo haziweza kudhuru viumbe wakubwa. Haidhuru wanyama na binadamu ikitokea ikaliwa, lakini vumbi lake lisivutwe/ kupumuliwa. Inaweza kutumika kama dawa ya kuulia wadudu kwa namna yoyote ile. Diatomite inachimbwa na kutengenezwa na kiwanda cha Diatomite kilichopo nchini Kenya katika eneo la Kariandusi, Gilgili pembezoni mwa Barabara iendayo Nakuru-Naivasha. Unaweza kuulizia na kupata aina ya Diatomite inayotumika kuulia wadudu. Mkulima anaehitaji anaweza kuwasiliana na idara ya masoko katika katika kiwanda hicho kwa anuani ifuatayo: Kiwanda cha Diatomite Afrika, S.l.p 32 Gilgili Kenya. Simu: 050-401 5209, +254 722 277 120.

Sabuni Unaweza kunyunyizia sabuni kwenye mimea yako dhidi ya vidukari, buibui, vitobozi, inzi weupe, viwavi jeshi, na katapila. Povu la sabuni: • Gramu 5-8 za sabuni kwenye lita ya maji huua vidukari na katapila wadogo • Gramu 8 za sabuni kwa lita ya maji huua katapila wakubwa • Gramu 10 za sabuni kwa lita zinaweza kuua mimea • Kamwe usitumie sabuni za unga (kama vile Omo): Zinaweza kuunguza majani ya mimea na kuathiri rutuba.

Maandalizi na matumizi 1. Yeyusha kijiko kimoja cha kulia cha sabuni ya kipande iliyokwaruzwa( Sunlight, Ushindi, n.k) kwenye lita 3 za maji (kupata dozi kamili tazama hapo juu) 2. Jaribisha kwanza kwenye mimea michache iliyoathiriwa. Kuwa makini na mimea inayoathirika haraka kama vile Kale. 3. Tumia kwenye mimea iliyo athiriwa ipasavyo, ukijumuisha sehemu ya chini ya majani ya mimea. Nyunyizia mapema asubuhi au jioni sana. Povu la sabuni linakuwa na ufanisi pale tu kunapokuwa na unyevu.


Madawa ya asili: Mwarobaini Dawa zinazotokana na mwarobaini zina ufanisi mkubwa sana katika kukabiliana na wadudu. Dawa nyingi za kuulia wadudu huwa na kiasi kikubwa chambegu za aina hii ya mimea. Mbali na kiasi kikubwa cha dawa hii, mwarobaini kwa kawaida haidhuru wadudu wa asili. Mwarobaini unatumika kama dawa ya kupaka na kama sumu. Inaondoa hamu ya wadudu ya kula, pamoja na kupunguza uwezo wao wa kutaga mayai. Mwarobaini hau uwi wadudu mara moja. Matokeo yake huonekana baada ya siku 10 tangu ulipotumika. Ili kuwa na mfanikio thabiti mwarobaini unatakiwa kutumika katika siku za mwanzo za kupambana na wadudu. Maji ya dawa yanayotokana na mbegu au majani ni mazuri zaidi kwa kupambana na viluwiluwi wa bungo, na katapila pia ni mazuri dhidi ya sota na bungo wakubwa. Bidhaa za mwarobaini zenye kiasi kikubwa cha mafuta zinaweza kuwa na madhara kwa mimea na kusababisha kuungua. Madhara yanayojitokeza hapo baadae kutokana na matumizi yasiyo sahihi yanakuwa makubwa. Kwa hiyo bidhaa zenye mafuta zinatakiwa kutumika kwa kufuata maelekezo. Zinakuwa na ufanisi mkubwa kwa kupambana na vidukari, inzi weupe, fukusi, panzi, na wengineo. Mafuta ya mwarobaini yanayotokana na mbegu, yanasaidia kulinda maharage yaliyohifadhiwa, kunde, na aina nyingine ya jamii za kunde kwa ufanisi. Mafuta ya mwarobaini pia yanaweza kutumika kama dawa ya fangasi.

Dawa ya Pareto Dawa ya Pareto inatokana na maua ya Pareto. Hii ni dawa ya kuulia wadudu ambayo ina uwezo mkubwa sana wa kuua aina nyingi za wadudu (Inajumuisha hata wadudu rafiki kwa mkulima) Kwa kuwa dawa inayotokana na pareto huua pale tu inapogusana na mdudu, ni vyema wadudu wanaoruka wakanyunyiziwa asubuhi na mapema wakati ambao bado hawajachangamka, na pia kabla nyuki wanaofanya ushavushaji hawajaanza kazi.

Pyrethroid Tofauti na ilivyo dawa ya Pareto, pyrethroids hii ni dawa inayokaa kwa muda mrefu sana na haitumiki kwenye kilimo hai. Pyrethroid (Mfano: Permethrin) inajumuisha Ammo, Ambush, Aztec, Pounce, na Warrior.

Maandalizi na matumizi ya Pareto

Tahadhari wakati wa maandalizi ya dawa ya mwarobaini Majani au mbegu zinaweza kuandaliwa kwa urahisi na wakulima. Ingawa siyo sumu kwa wanyama, lakini mbegu zake au kinachotokana na mbegu ni sumu kinapoliwa. Chukua tahadhari zifuatazo: • Weka mbali na watoto pamoja na wanyama wa ndani kama vile paka na mbwa, wakati wa maandalizi, matumizi na hata kuhifadhi. • Epuka kugusa mafuta yanayotokana na mbegu hizo moja kwa moja wakati wote. • Usitumie vyombo vya jikoni au vya kulia, au kunywea wakati wa maandalizi ya dawa. • Safisha vyombo vyote sawa sawa kabla na baada ya kuvitumia kwa maandalizi. • Osha mikono yako vizuri baada ya kushika dawa. • Wakati wote kumbuka kujaribisha kwanza dawa kwenye mimea michacheiliyoathirika kabla ya kunyunyiza katika eneo kubwa. • Tumia mavazi maalumu ya kujikinga unaponyunyiza.

Namna gani ya kutengeneza maji ya dawa kutokana na mwarobaini 1. Okota matunda yanayodongoka kutoka kwenye mwarobaini. 2. Menya matunda hayo na uoshe ili kubaki na mbegu tu. 3. Kausha mbegu zikiwa kwenye mfuko au kwenye kikapu. Epuka mkandamizo utakaosababisha kubadilisha muonekano wa mbegu hizo. 4. Kutengeneza dawa ondoa makaka yote. 5. Saga gramu 500 za mbegu za mwarobaini katika kinu, mashine au kwa njia nyingine yoyote itakayosaidia kufanya ziwe laini. Changanya mbegu ulizosaga kwenye lita 5 mpaka 10 za amaji. Loweka usiku wote. 6. Chuja kabla ya kutumia.

Matumizi • Nyunyiza maji ya dawa moja kwa moja kwenye mimea kwa kutumia bomba au brashi. • Dawa ya mwarobaini hufanya kazi haraka wakati wa joto. Mvua inaweza kusafisha dawa ya mwarobaini kutoka kwenye mimea. Rudia kunyunyiza endapo wadudu bado wanaonekana kuwepo kwa wingi kwenye mimea yako. • Dawa hii itaendelea kuwa na nguvu kwa muda wa siku 3-6 endapo itahifadhiwa kwenye giza. Dawa yoyote ya mwarobaini inapokuwa ilishaandaliwa hupoteza nguvu haraka inapowekwa kwenye mwanga wa jua.

Unga wa Pareto na kunyunyiza

Chukua tahadhari sawa na ulivyofanya kwenye maandalizi ya mwarobaini. Pareto na mbegu zake ni sumu kwa viumbe jamii ya mamalia. Ukishika na kugusana na ngozi kwa muda mrefu inaweza kusababisha harara, kuvuta kwenye hewa au kunyunyiza ikiwa kwenye unga inaweza kusababisha maumivu ya kichwa, kuumwa au kuibua mzio (allergy).

Chuma maua yanapokuwa yamechanua vizuri, yakaushe sehemu yenye kivuli na uhifadhi sehemu yenye giza. Pareto huharibiwa haraka sana na mwanga wa jua. Inafanya kazi vizuri zaidi kwenye joto la chini, kukiwa na mawingu, na ufanisi wake hupungua inapotumika wakati wa mchana au wakati wa joto kali. Kama ukiona wadudu wanarudia hali yake ya kawaida baada ya muda fulani, basi inahitajika dawa kali zaidi.

Maandalizi ya unga wa pareto na sabuni

Kunyunyizia dawa ya pareto

Maua yaliyolowekwa kwenye maji yanadhibiti vudakari na buibui vizuri sana. • Vikombe 2 vya maua yaliyosagwa vizuri vinachanganywa kwenye lita 5-10 za maji • Changaya vijiko 2 vya sabuni kisha ukoroge. Koroga mchanganyiko uliochuja kabla ya kutumia. Nyunyiza wakati wa asubuhi na uhakikishe unanyunyiza upande wa chini wa majani pia. Wakati wa mchana, mchanganyiko huo utakauka, wadudu hujikunja kisha kufa.

Weka maji lita 1 kwenye vikombe viwili vya maua mabichi ya pareto (au nusu kikombe cha unga wa pareto) loweka kwa masaa machache. Chuja na uchanganye na sabuni na uchanganye lita 2-5 za maji. Ili kuwa na matokeo mazuri zaidi nyunyiza wakati wa jioni. Unga wa pareto Saga maua yaliyokauka na unga wa pareto. Tumia ukiwa halisi hivyo au na kitu kingine kama vile limao au diatomite. Nyunyiza kwenye mimea iliyoathiriwa.


Dawa za ukungu

Zingatia:-Unapotumia dawa za ukungu, hatua za usalama ni lazima zifuatwe kwa usahihi. -Soma maelekezo kwa uangalifu. Kipimo na maelekezo kabla ya muda unaotakiwa kuzingatiwa

kabla ya kuvuna.

-Muulize mtaalamu wa kilimo aliekaribu nawe juu ya dawa za ukungu zinazopatika katika eneo lako. -Usile, kunywa au kuvuta wakati umeshika au kutumia madawa ya mimea ikiwemo copper.

Dawa za ukungu zinazotokana Dawa za ukungu zinazotokana na madini: Kopa na madini: Salfa Kopa ni dawa yenye nguvu sana dhidi ya ugonjwa wa ukungu. Dawa ya kopa bado Salfa inatumika kwenye kilimo cha mbogamboga, maua, matunda na mazao ya muda mrefu kutibu ugonjwa wa kimamba, kutu, madoa kwenye majani, na kuoza matunda. Pia inatumika kama dawa ya kudhibiti wadudu kama vile buibui. Salfa siyo sumu kwa jamii ya mamalia, lakini inaweza kusababisha muwasho wa macho na ngozi. Inaweza kusababisha madhara kwa mimea hasa wakati wa kiangazi kukiwa na joto zaidi ya nyuzi joto 32°C. Haiwezi kutumika pamoja na aina nyingine za dawa. Salfa ikichanganywa na dawa zenye mafuta hutengeneza vimelea vya sumu inayojulikana kama phytotoxic.

Salfa na chokaa Mchanganyiko huu hutumika kwenye miti ya matunda ili kudhibiti ugonjwa wa ukungu na wadudu. Hii ni sumu na inaweza kuchoma ngozi na macho, inaweza kudhuru mimea endapo itatumika kukiwa na joto linalozidi nyuzi joto 26°C, na ina harufu ya mayai viza. Chukua tahadhari unapotumia salfa na chokaa.

inatumika katika kilimo hai, lakini kiwango cha matumizi bado kinazingatiwa kwa kuwa hukaa katika udongo kwa muda mrefu na inaweza sababisha madhara. Mchanganyiko wa Bordeaux hii hudhibiti bakteria wanaosababisha madoa kwenye majani, madoa yanayosababishwa na bakteria, mnyauko, kimamba, kutu kwenye majani, canker na mengineyo. Pia inafukuza aina nyingi za wadudu. Inatumika kwa mboga, miti ya matunda. Kama ilivyo kwa salfa, inaweza kutengeneza vimelea vya sumu kwa mimea, hasa kama itatumiwa wakati wa unyevunyevu au wakati wa baridi. Kama mahitaji yanapatikana inaweza kutengenezwa nyumbani kwa urahisi. Chukua tahadhari zote zilizoelekezwa kwa dawa ya mwarobaini.

Kunyunyizia mchanganyiko wa Bordeaux -Vijiko 3½ vya kulia vya kopa -Vijiko 10 vya kulia vya chokaa -Galoni 1 (ya lita 4) za maji kwenye chombo cha plastiki Ongeza kopa na chokaa kwenye maji na ukoroge vizuri kwa kutumia kipande cha mti. Jikinge na uepuke kugusana na mchanganyiko huo. Matumizi -Tikisa bomba la kunyunyizia mara kwa mara ili kuepuka mchanganyiko huo kuganda -Nyunyizia mimea kwa ukamilifu, inapendekezwa iwe asubuhi wakati wa kiangazi au siku kuna jua. Kwa njia hii, mimea inapata nafasi ya kukauka na dawa haiwezi kupata nafasi ya kupenya kwenye matundu ya majani ya mimea.

Ni kwa jinsi gani mbegu zinatibiwa kwa maji ya moto Kutibu mbegu kwa kutumia maji ya moto huzuia magonjwa ya mbegu kama vile kuoza, kuweka uozo mweusi, na kuoza kwenye kikonyo. Kuimarisha ubora wa mbegu, uwiano wa muda, na hali joto ni lazima vifuatwe kwa makini! Unahitaji kuwa na kipima joto kizuri au kuomba usaidizi kutoka kwa mtaalamu wa kilimo aliefuzu.

1. Injika chungu/sufuria kubwa kisha jaza maji, na uyachemshe kufikia kiwango cha joto kinachohitajika (tazama jedwali hapo chini) 2. Weka mbegu kwenye mfuko uliotengenezwa na kitambaa cha pamba ukiwa haujafungwa sawa sawa kisha tumbukiza kwenye maji hayo. Koroga maji hayo mfululizo huku ukiwa umeloweka mfuko huo. Kamwe mfuko huo usiguse sehemu ya chini ya chungu/sufiria. 3. Baada ya muda unaohitajika (tazama kwenye jedwali) toa mfuko huo na mara moja uweke kwenye maji ya baridi ili kuondoa joto. 4. Sambaza mbegu hizo kwenye jamvi lililo safi ili kuzipooza na kukausha 5. Mbegu ni lazima zipandwe mara moja kwenye kitalu ambacho kimeshaandaliwa

Kiwango cha hali joto na muda unaopendekezwa kwa kutumia maji ya moto kutibu mbegu Mbegu Hali joto Viazi 55°C Spinachi, kabichi, pilipili, nyanya, biringanya 50°C (122 F) Broccoli, cauliflower, karoti, collard, kale, kohlrabi, turnip 50°C Haradali, cress, radis 50°C Mchicha, celery, celeriac 47°C Maotea ya ndizi (Fukusi na Minyoo) 52°C-55°C Maotea ya nanasi (mealybugs, Phytophthora na minyoo) 50°C

Muda Dakika 10 Dakika 30 Dakika 20 Dakika 15 Dakika 30 Dakika 20 Dakika 30

Moduli hii imechapishwa na Mkulima Mbunifu kwa ushirikiano na The Organic Farmer (info@organickenya.org, P.O. Box 14352-00800 Nairobi, Kenya, +254 20 440398), Biovision Africa Trust, www.biovision.ch

Imeandaliwa na Theres SZekely na kutafsiriwa na Ayubu Nnko Mkulima Mbunifu: S.L.P. 14402 Makongoro Street Arusha Rununu: 0717 266 007, 0785 133 005 www.mkulimambunifu.org Barua pepe: info@mkulimambunifu.org


Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.