7 minute read
OPERESHENI DAKABU by Joseph Shaluwa
To make your ferry journey fly by, here is a gripping short story to read. Joseph Shaluwa is a Tanzanian writer known for his page-turning works full of intrigue and suspense. Operesheni Dakabu (Operation Dakabu) is a short story specially written for Jahazi by Joseph and centres on Inspector Mark, who, the day after getting married, is tasked with uncovering a plot to stage a political riot. Enjoy!
MUITO wa simu iliyokuwa mezani ulimgutusha pale kitandani alipokuwa amelala, lakini aliipuuza. Simu kwa wakati ule haikuwa na maana kabisa kwake.
Msichana mrembo Upendo, alikuwa kando yake, akionyesha kumhitaji sana ndiye aliyekuwa na maana na thamani kuliko chochote. Ilikuwa ni asubuhi ya kwanza kwao kama wanandoa. Kwa miaka mitatu ya uchumba, hawakuwahi kulala hadi asubuhi hata mara moja.
Ilikuwa siku yao muhimu sana. Mark alimgeukia Upendo, kisha akamwambia: “Kuna watu wanaojua kuharibu starehe za wenzao. Hivi ni nani ambaye hajui kuwa jana nimetoka kuoa?
“Nani ambaye hajui kuwa nipo fungate na mke wangu tukitafuta mtoto?”
Upendo akabaki anamwangalia tu usoni bila kujibu. Pengine angalia yake ilikuwa jibu tosha, kwamba anamsuta kwa kitendo chake cha kutokuwa mwerevu.
“Mbona hujibu kitu?” akauliza Mark.
“Unashindwa nini kuizima?”
“Lakini mke wangu Upendo, mara hii umesahau kuwa mimi ni polisi?”
“Kwahiyo?”
“Muda wote nipo kazini!”
Eti muda wote nipo kazini! Akawaza
Upendo akimkata Mark jicho la kebehi.
Mark alielewa alichokuwa akimaanisha mkewe. Alimhitaji faraghani. Akiwa mawazoni, simu ikaita tena. Mara moja akaichukua...
Paaa! Moyo wake ukashtuka. Ilikuwa simu kutoka ofisini – Makao Makuu – kwa bosi wake – Mkuu wa Kitengo cha Kazi Maalum.
Kitengo hiki kilisimamiwa na Mkurugenzi wa Upelelezi Maalum, Kamishna Msaizidi wa Polisi (ACP), Kelvin Kayanda. Kilifanya kazi kwa karibu na idara ya Usalama wa Taifa.
Tofauti ya kitengo hiki na vingine vilivyopo kwenye Jeshi la Polisi, huripoti moja kwa moja kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Kwa kawaida, kitengo hiki hufanya kazi ya kuhakikisha inachunguza, inathibiti na kuwakamata wanaohusika na uharibifu wa amani ya nchi.
Kupigiwa simu moja kwa moja na ACP Kelvin Kayanda kulimpa picha Mark, kuwa kulikuwa na jambo zito linalohitaji usaidizi wake. Hapo akawa na uhakika kuwa fungate imeshaharibika.
Mara moja akapokea!
“Jambo!” sauti nzito ya ACP Kelvin Kayanda ilisikika kutoka upande wa pili.
“Jambo afande.”
“Najua upo fungate, lakini kwa ajili ya taifa lako, nakuomba ofisini ndani ya saa mbili kutoka sasa, asante sana,” akasema ACP Kayanda, kisha akakata simu.
Ulikuwa wito wa dharura. Amri. Hapakuwa na majadiliano. Insp. Mark akabaki anaitazama ile simu kwa ghadhabu, kisha akamgeukia mkewe na kumwambia: “Samahani mpenzi, ni simu kutoka ofisini. Amenipigia bosi mwenyewe. Natakiwa kazini sasa hivi.”
“Nilijua tu.”
“Samahani mpenzi wangu.”
“Itanisaidia nini.”
Insp. Mark hakuwa na muda wa kubembelezana na mkewe. Alitakiwa kuifikiria nchi kwanza kabla ya ndoa yake. Ndiyo kiapo chake kilivyokuwa. Akajitoa kitandani na kujiandaa.
Kama Upendo ataniacha kwa ajili ya kazi na aniache tu! Akawaza Mark akimalizia kufunga mkanda.
“Kitu kimoja cha muhimu unatakiwa kufahamu, nakupenda sana Upendo. Lakini ndoa yetu, maisha yetu hayatakuwa na maana bila kazi. Acha nikafanye kazi,” akasema Insp. Mark akimwangushia mkewe busu mwanana.
Upendo hakujibu, aliishia kulia.
Inp. Mark hakujali.
Akaondoka zake.
INSP. Mark alimalizia kupandisha ngazi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam. Alitembea mpaka kaunta, kisha akakata kulia na kupandisha ngazi kuelekea ofisini kwa ACP Kelvin Kayanda.
Uzuri ni kwamba, hoteli waliyoamua kukaa kwenye fungate lao la kwanza, ilikuwa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, alipotokea, ilikuwa wakae hapo kwa wiki moja kabla ya kwenda Visiwani Comoro kumalizia fungate lao.
Lakini kwa sababu ya kazi, amelazimika kumuacha mkewe mbichi, Upendo na kwenda kazini. Alipoufikia mlango, akagonga mara moja na kuingia.
“Nimefurahi umeitikia wito, tena kwa wakati. Nisikupotezee muda. Unatakiwa kusafiri leo kwenda Kahama. Tumeshaandaa ndege kwa ajili ya safari hiyo. Maelekezo yote ya safari yako, yapo humu kwenye hii bahasha,” akasema ACP Kelvin Kayanda akimkabidhi
Insp. Mark bahasha kubwa ya kaki.
“Dereva wa kukupeleka airpot yupo nje anakusubiri. Ndege yako ipo. Ukifika utapokelewa airpot. Kazi njema.”
“Asante afande. Kinachofuata?” “Asante afande,” akasema Insp. Mark akisimama na kupiga saluti, kisha akaondoka zake.
KWA mara ya tatu sasa, Insp. Mark alikuwa akirudia kusoma maelezo ya kazi aliyopewa akiwa kitandani, hotelini kwake, mjini Kahama.
Kila alipokuwa akitafakari namna ya kumpata mtuhumiwa huyo aliyejulishwa alikuwa mjini Kahama, akili yake ilimkataza kuamini hilo.
“Hawezi kuwa mjinga, aje hapa Kahama kweli kama walivyopanga. Hawezi kuwa hapa. Aliiamini akili yake, akaamua kufanyia kazi mawazo yake. Hata hivyo hakutaka kumshirikisha bosi wake. Kwa sababu hiyo, jioni hiyohiyo alipanda basi la Kandahari Express lilikuwa likitokea Moshi, kuelekea Bukoba.
“Hata kama hatakuwa Bukoba, anaweza kuwa anajaribu kuvuka mpaka wa Mutukula kuelekea Uganda au ameshavuka kabisa,” akawaza Insp. Mark.
ALIFIKA Bukoba usiku, akafikia Hoteli ya Vicktoria, iliyokuwa jirani kabisa na Ziwa Vicktoria, katika barabara kuu ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Alilala mpaka asubuhi ambapo aliamkia kuhangikia kazi iliyompelekea mjini humo. Katika nusa nusa yake, aliona mwanga, lakini hakuelewa namna ya kumkamata mtuhumiwa.
Usiku aliamua kwenda kwenye klabu ya usiku ya Mint. Si kwa lengo la kustarehe, alielewa kwenye changanyikeni ya watu, huenda angepata cha maana kwenye upelelezi wake.
Ndani ya klabu, akamuona msichana mmoja aliyekuwa akitumia fedha nyingi sana na marafiki zake. Meza yao ilichafuka pombe za bei mbaya. Akasogea jirani na meza hiyo, kisha akawasalimia wote, wakamwitikia kwa dharau.
Akamuita mhudumu na kuwaagizia wote vinywaji. Bili ilikuwa laki tatu na nusu. Akalipa keshi. Hapo akakaribishwa ramsi katika meza hiyo.
“Naitwa Sasha,” akajitambulisha yule msichana aliyekuwa bosi wa meza ile.
“Mimi ni Joe,” akadanganya jina lake.
“Nice name!”
“Hata lako pia.”
Mazungumzo yakaendelea, baadaye wakawa marafiki wakubwa kama waliokutana muda mrefu kabla. Sasha alipoanza kulewa, akaanza kumtazama Mark kwa jicho la tofauti. Ulipofika muda wa kucheza muziki laini, Mark akaitumia nafasi hiyo vizuri. Sasha akalainika.
“Siamini kama moyo wangu unanidanganya, but I am crazy with you darling. Please be with me tonight,” akasema Sasha kwa sauti iliyojaa mahaba.
“You are welcome baby,” akasema Mark.
Mzozo ulikuwa nani alale kwa mwenzake. Sasha alijitambulisha kama mgeni wa mji wa Bukoba akitokea Dar es Salaam na Mark akasema yeye ni mgeni kutokea Kahama, akiwa mfanyabiashara wa madini.
Kila mmoja alitaka mwenzake afikie kwenye hoteli yake, mwishowe Sasha alishinda. Wakaelekea hotelini kwake – Gunda Hotel.
UMAKINI ulikuwa mkubwa kwa Insp. Mark. Hakuyapa mapenzi kipaumbele, kwa sababu hakuwa pale kwa sababu ya mapenzi, bali kazi.
Alimhadaa Sasha, akapitiwa na usingizi. Alichokifanya Insp. Mark ni kumnusisha dawa za usingizi, Sasha akalala maradufu. Insp. Mark akatumia muda huo vizuri kumchunguza.
Sasha alikuwa na nyaraka nyingi za siri. Alitumiwa na chama kimoja cha siasa kuharibu amani ya nchi. Shasha alikuwa ndiye mhifadhi mkuu wa nyaraka zote siri. Walimtumia yeye kutokana na mwonekane wake.
Waliamini uzuri wake unaweza kuwapumbaza polisi wasimhisi. Haikuwa kwa Insp. Mark. Baada ya kukamilisha vielelezo vyote, alivipiga picha kisha akavirudisha alipovitoa.
Asubuhi Sasha aliamka akiwa hoi. Akiwa na akili zake, asubuhi hiyo alimuona Insp. Mark katika mwonekano mpya zaidi. Alimuona angefaa kuwa mumewe.
“Natamani unioe, Joe.”
“Hata kesho nipo tayari.”
“Basi nipeleke kwa wazazi wako.” “Wapo Dar es Salaam, twende wikiendi.” “Sawa.”
NDEGE ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jioni hiyo.
Insp. Mark (Joe) na Sasha walikuwa miongoni mwa abiria wa mwanzo kushuka kwenye ndege hiyo. Wakatembea wakiwa wameshikana mikono.
“Wifi zako wamekuandalia zawadi nzuri sana,” akasema Insp. Mark.
“Nakuamini Joe... na kwakweli nimekuamini mapema sana mpenzi.”
“Usijali, hata mimi pia mpenzi.”
Wakatembea wakitoka kwenye lango kuu la abiria wanaowasili. Wakatembea hadi kwenye maegesho, gari jeusi aina ya Benz, lilikuwa limeegesha linawasubiri. Insp. Mark akafungua mlango wa nyuma, Sasha akaingia.
Sasha alipoingia tu, askari wawili wa kike waliovalia suti nyeusi, waliingia kila upande. Akakaa katikati. Insp. Mark akaketi siti ya mbele.
“Hao ndiyo wifi zako, Sasha,” akasema Insp. Mark akitabasamu.
“Upo chini ya ulinzi, hutakiwi kujigusa wala kujaribu kufaya fujo yoyote,” akasema mmoja wa askari wale.
Stupid! Sasha akaachia tusi moyoni.
“Joe umeniuza? Oh! My God.”
“Sasha, my name is Insp. Mark, and I am not Joe, as I told you before. Upo chini ya ulinzi na unachotakiwa kufanya ni kutaja listi ya wenzako wote mnaojaribu kupanga mipango ya kuihujumu nchi iingie kwenye machafuko,” akasema Insp. Mark.
“Hata nife, siwezi kuwataja.”
“Na utakufa kweli, pumbavu wewe!” akasema Insp. Mark.
Ni Operesheni Dakabu – Dar es Salaam, Kahama, Bukoba. Safari ya kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam ikaanza.
JOSEPH SHALUWA ni mtunzi wa riwaya za Kiswahili, nchini Tanzania. Kama unahitaji vitabu vyake, wasiliana naye kwa namba 0718-400146, 0786224191, joeshaluwa@gmail.com, Facebook: Joseph Shaluwa. Instagram: @joeshaluwa