Jarida la kilimo endelevu Afrika Mashariki Kuna msemo usemao, “kinga ni bora kuliko tiba.� Ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kupingana na usemi huu kwa kuwa umejaa ukweli. Wakulima na wafugaji walio wengi wamekuwa wakipata hasara ambayo mara nyingi hawajui chanzo chake. Hasara hiyo inaweza kuwa katika hali tofauti, ikiwa ni pamoja na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kutibu mifugo ama kununulia dawa za kuulia wadudu shambani. Pia inaweza kuwa hasara inayotokana na mifugo kufa au mimea kuharibiwa na wadudu au magonjwa. Jambo hili linaweza kuepukika endapo mkulima ataweza kuweka mazingira yake katika hali ya usafi. Hii ina maana kuweka shamba katika hali ya usafi ili kuepukana na shamba lako kuwa makazi ya wadudu waharibifu na hali kadhalika kuwa maficho ya vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa. Ondoa magugu na vichaka vyote shambani mwako kila yanapomea. Endapo utaweka shamba lako katika hali ya usafi wakati wote na kufuata taratibu zinazoshauriwa kitaalamu basi utaweza kuepuka hasara inayotokana na mazao yako kushambuliwa na wadudu au magonjwa. Hili si kwa mimea tu bali pia kwa mifugo. Endapo atawaweka wanyama katika mazingira chafu, hakika hautaweza kuepuka hasara kwa kuwa wanyama wataugua mara kwa mara na hata kufa. Pia utatumia gharama kubwa katika kununua madawa ili kutibu na kulipia gharama za matibabu kwa mifugo. Hakikisha kuwa banda na mazingira ya wanyama ni safi na salama ili kuepuka magonjwa pamoja na
wadudu wanaoweza kusababisha magonjwa, hali kadhalika minyoo. Ukiwa na mifugo wenye siha nzuri ni dhahiri kuwa una uhakika wa kupata faida kwa kuwa hakuna gharama utakayotumia kuhangaikia matibabu, na hata utakapotaka kuuza mifugo wako watakuwa wakivutia na kuweza kukupatia hela nyingi bila shida.
Unaweza kufaidika kwa kulima kibiashara Ni wazi na inatambulika kuwa kwa sasa ulimwenguni kote kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira, na kutoa mchango mkubwa katika kuondoa umasikini. Hivi sasa serikali na wadau mbalimbali wanahimiza wakulima kuangali kilimo katika mtizamo wa kibiashara. Kuanzisha kilimo cha biashara ni tofauti na kulima tu kawaida, kupanda na kuvuna, mambo yakaishia hapo. Kuna vitu vingine vingi vya kufikiria mbali na udongo pamoja na matunda yake. Kuweza tu kutambua ni aina ipi ya kilimo inaweza kufanyika kibiashara
haitoshi. Huo ni mwanzo tu. Ni lazima kukusanya pesa ili kuwa na mtaji ambao utawezesha kufanya kilimo kibiashara na mwishowe uweze kupata faida zaidi. Inashauriwa kuwa mkulima aanze kwa kuwaza upatikanaji wa soko kwa ajili ya mazao yake. Kisha azalishe mazao bora kwa ajili ya soko hilo. Wote ambao wamekubali mabadiliko haya na kuzingatia taaluma na usimamizi mzuri wa kibiashara sasa wanapata faida nzuri. Wameweza kuziba mianya yote ambayo ingesababisha kupoteza pesa. Soma uk. wa 8.
Toleo la 4
Januari, 2012
Uvunaji wa maji Soya zao maridhawa
2 7
Kilimo ni biashara
8
Hivi sasa duniani kote tatizo la ajira limekuwa ni wimbo wa kila mtu, ambao si wa kufurahisha bali unaotia uchungu, simanzi na kuumiza. Hii inatokana na ukweli kuwa sehemu kubwa ya kazi zilizokuwa zinafanyika kwa kutumia mikono na hata zile za kitaalamu zimechukuliwa kwa sehemu kubwa na maendeleo ya kupanuka kwa teknolojia, lakini pia kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia, ambapo watu wengi wamepoteza ajira, ambazo haziwezi kufidiwa na masuala ya kisiasa ama biashara. Jambo kubwa la kutia moyo na kufurahisha ni kwamba kuna eneo moja ambalo linaweza kutoa ajira ya kueleweka na kuaminika. Eneo hilo ni katika shughuli za kilimo na ufugaji. Watafiti wa shughuli za kilimo wanasema wakaazi wengi wa nchi za Afrika na maeneo mengine duniani hawakuwa wakithamini kilimo, lakini waliojaribu wamepata mafanikio makubwa na hata kuajiri watu wengine kusaidia kuendesha shughuli za Kilimo. Unaweza kuona ukweli wa jambo hilo kwa kuchukua mfano rahisi, jinsi mzunguko wa shughuli za kilimo na ufugaji unavyoweza kutengeneza ajira kwa watu wengi. Mkulima ataanza kwa kulima mboga mboga, wakati wa kuandaa shamba huenda akataka msaidizi ambaye atajipatia ujira, kisha mkulima atanunua mbegu, ambapo yule anayeuza amepata kipato. Baada ya muda atapata mavuno na ataweza kuuza kwenye mahoteli, masoko na maduka makubwa, ambapo kuna watakaopata ajira kutokana na mkulima huyu ambaye asingekuwepo watu wote katika mzunguko huo wasingekuwa na kipato. Si tu katika mzunguko wa uzalishaji wa ajira kupitia kilimo cha mazao ya chakula, lakini pia viwanda vinategemea malighafi yanayotokana na kilimo kwa mfano katani, pamba, kahawa, na hata kupata nishati mbadala inayotokana na mimea kuendeshea mitambo. Ni vyema sasa tukaamka na kuthamini shughuli za kilimo kuliko ambavyo baadhi ya watu wanachukulia kuwa ni shughuli za kimasikini ama watu wasiokuwa na mwelekeo mzuri kimaisha. Bila wakulima na wafugaji, hakuna hata mmoja atakaeweza kuishi na kufanya shughuli nyingine kwa kuwa wote tunategemea shughuli za kilimo kujipatia chakula na mahitaji mengine muhimu.
Mk M, S.L.P 14402, Arusha, Simu 0717 266 007, 0785 133 005 Barua pepe info@mkulimambunifu.org, www.mkulimambunifu.org