Moduli 5, Mboji, samadi na mbolea maji (revised)

Page 1

Mkulima Mbunifu Moduli namba 5

MBOJI, SAMADI NA MBOLEA MAJI Mboji inahusika moja kwa moja na kilimo hai. Sehemu ya kutengenezea mboji ni muhimu sana kwa kuwa mbolea yote inayozalishwa shambani ndipo hukusanywa, kuozeshwa kwa ajili ya mimea, na kurudishwa kwenye mzunguko wa virutubisho kama mbolea na njia ya kufufua udongo uliochoka. Mboji ni uwekezaji wa muda mrefu kwenye udongo. Inaongeza rutuba kwenye udongo kwa kuongeza viini vya asili, na kuimarisha muundo wa udongo, na kutoa virutubisho kwa mimea ambavyo hutolewa taratibu na kwa muda mrefu.

Kuoza, njia ya asili Viumbe hai vyote, iwe mimea au wanyama, vitaoza vitakapomaliza mzunguko wa uhai/maisha yao. Kazi hiyo ni jukumu kubwa la viumbe hai vidogo sana ambavyo haviwezi kuonekana kwa macho na vipo katika mazingira yetu, kwenye udongo, kwenye maji, na hata katika hewa. Bila wao, maisha duniani yasingewezekana. Mamilioni ya viumbe hawa wanaweza kupatikana katika kiganja cha udongo wenye rutuba. Kuozesha ni njia tu ya kuhamasisha njia hii ya kutengeneza mbolea na kuwa na tumaini la kuwa na mbolea nzuri. Matokeo ya muozo unatokana na malighafi hai zilizopata unyevu. Mbolea hiyo huupa udongo rangi nyeusi na si rahisi kuoza zaidi.

Mbolea asili huboresha rutuba kwenye udongo Kutumia mboji huongeza rutuba kwenye udongo baada ya muda mrefu. Hii ni sehemu na matokeo ya mbolea za asili: • Zinachukua na kuhifadhi kwa kiasi kikubwa sana cha virutubisho na chembechembe ndogo muhimu kwa ukuaji na ustawi wa mimea. • Zinaweka na kuhifadhi maji, na kuyafanya yapatikane kwa ajili ya mimea kwa kipindi kirefu. • Zinaboresha muundo wa udongo na kuukinga dhidi ya mmomonyoko unaosababishwa na maji na upepo.

Mbolea za asili na zisizo za asili Mbolea za asili kama vile mboji na samadi, aina kuu ya virutubisho vya mimea, nitrojeni (N) fosiforasi (P), na Potashiamu (K) na aina nyingine za virutubisho zimefungamanishwa kwenye mbolea za asili na huachiliwa kwa ajili ya mimea taratibu. Mbolea zisizo za asili kwa kawaida huwa na Nitrojeni, fosiforasi, na potashiamu, kwa kiwango kikubwa sana. Zinayeyuka kirahisi kwenye maji na kunyonywa haraka. Hata hivyo kutumia mbolea za viwandani peke yake hakuimarishi rutuba kwenye udongo na kuna hatari ya kusababisha tindikali (acid) kwenye udongo. Mbolea za asili zinahitajika kwa ajili ya kuhifadhi virutubisho na maji kwenye udongo. Mbolea zisizo za asili zinapotumika mkulima pia anahitajika kuzingatia kiwango cha malighafi na mbolea za asili kwenye udongo. Mbolea za asili ni muhimu sana hasa katika uzalishaji wa mboga. Aina nyingi za mboga hufanya vizuri kwenye udongo ambao una mbolea ya asili ya kutosha, mfano mnafu, kabichi, matango, au magimbi. Kwenye udongo wa aina hii mimea huvumilia minyoo ambayo ingeweza kuwa tatizo. Moduli ya MkM namba 4 (Virutubisho vya mazao ya asili) inakupa taarifa zaidi juu ya mbolea za asili na matumizi yake.

“Mboji” ina maanisha mkusanyiko, mchanganyiko. Karibu malighafi zote za mimea ya asili zinaweza kutumika kutengeneza mboji. Kutoka shambani na bustanini Mabaki ya mazao, magugu, majani yaliyodondoka, kukata matawi (aina yoyote ya mimea)

Kiasi kikubwa cha mimea yenye magonjwa inapendekezwa kuozeshwa kwa kutumia njia ya joto (Njia nzuri, tazama ukurasa unaofuata)

Kutoka kwenye banda la mifugo Samadi na mkojo, matandiko, na mabaki ya malisho. Kutoka nyumbani

Mabaki ya jikoni, maji yanayotumika nyumbani, majivu ya kuni, taka zilizofagiliwa nyumbani, na karatasi zilizochanwa chanwa.

USITUMIE:

Mabaki ya nyama (yanavutia panya na wadudu wengineo, mbwa na wanyama wa mwitu) Malighafi zisizo za asili kama plastiki na vyuma laini.


TEKELEZA!

Hauhitaji kufahamu zaidi ya kanuni tatu!

Uozeshaji hufanyika kwa kupitia mamia ya njia duniani kote. Njia zote hizi zinaweza kugawanywa katika makundi mawili:

Sehemu yenye kivuli. Hii ni muhimu ili kuzuia malighafi zako zisikaushwe na jua. Chagua sehemu iliyopo chini ya miti au kuwa na vichaka, katikati ya migomba au sehemu yenye paa.

Njia mbalimbali za kupata mboji nzuri -Kuendelea kurundika (Njia rahisi zaidi) Taka zote za asili hurundikwa mahali pamoja kwenye rundo kadri zinavyozalishwa na kupatikana katika kipindi chote cha mwaka. Kwenye rundo hilo, kiasi cha joto hakiwi juu ukilinganisha na rundo ambalo limetengenezwa mara moja, na kwa maana hiyo uozaji hutokea taratibu zaidi. -Kurundika kwa matabaka (njia nzuri zaidi) Malighafi hukusanywa tofauti tofauti, kisha kuchanganjwa na kurundikwa mara moja. Utaratibu huu hufanya kuwepo na joto kali katika hatua za uozaji. Faida yake ni kwamba husaidia kuzuia upotevu wa virutubisho, kuharibu vimelea vya magonjwa, na mbegu za magugu ikiwa ni matokeo ya joto kali. Mboji inakuwa tayari baada ya kipindi kifupi sana na inakuwa na ubora wa hali ya juu.

Kama ukizingatia na kushika kanuni hizi, utapata mbolea mboji bora na kwa kiwango cha kutosha.

Fanya malighafi zako ziwe na unyevu. Mbinu zote zitafanya: • Mbinu zote zitafanywa: • Wakati wa kiangazi, nyunyizia maji. • Funika mboji yako kwa kutumia majani ya migomba au karatasi ya nailoni muda wote. • Kwenye sehemu kame, tumia shimo lenye urefu wa futi 1-2 ili kuhifadhi unyevu vizuri. • Au unaweza kufunika rundo ambalo limeshaiva kwa kutumia matope yenye unene wa sentimita 15. Kinga mboji yako dhidi ya mvua Ili kuzuia virutubisho kama nitrojeni na potashiamu kutiririshwa na maji una sehemu ambayo ipo chini ya paa, ni vizuri zaidi, kwa karatasi ya nailoni itafanya vizuri na kuwa na matokeo yanayofanana.

Njia rahisi ya kutayarisha mboji Kama una malighafi nyingi sana, geuza na usogeze rundo hilo mara tu litakapofikia urefu wa mita moja. Kisha anza rundo lingine. Kama hili pia likifikia urefu wa mita moja, geuzia malighafi hizo kwenye rundo la kwanza, funika na uanze kukusanya tena. Kwa njia hii, muda wote utakuwa una mbolea iliyopo tayari kwa matumizi.

Kutengenezea mboji karibu na banda la mifugo

Njia rahisi ya kuandaa mboji ni kukusanya malighafi mfululizo. Tupa aina zote za taka zinazooza kwenye rundo moja. Geuza, changanya na uhamishe rundo hilo mara moja tu, kisha liache hapo mpaka utakapolihitaji kwa ajili ya mbolea. Wakati mzuri wa kugeuza rundo ni miezi miwili au mitatu kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua. Mboji itakuwa tayari utakapoihitaji kwa ajili ya kupandia. Baada ya kuligeuza rundo lifunike na uliache liive vizuri. Kuanzia sasa na kuendelea, aina mpya ya malighafi hukusanywa katika rundo jipya. Unaweza kutumia mahali au shimo ulipoondoa mboji ulipogeuza.

Kama unafuga (Ng’ombe, mbuzi, kondoo, sungura, kuku) kwenye sehemu iliyofungwa na samadi hudondokea sehemu moja, rundo, au shimo linatakiwa kuwa hapo karibu. Pia kusanya aina nyingine ya taka zinazooza mahali hapo. Inashauriwa kuongeza matandiko mengine (mabua ya mahindi, magugu, majani n.k) kwenye banda la mifugo kila wiki ili yalowanishwe na mkojo na kinyesi cha wanyama. Banda ni lazima liwe na paa ili mkojo na kinyesi visitiririshwe na mvua. Mabaki ya malisho, matandiko, kinyesi na mkojo vinaongezwa kwenye rundo mara kwa mara. Unaweza kutumia njia rahisi mfano kukusanya taka zote zinazooza kwenye shimo moja mpaka zifikie urefu wa mita moja, kisha zigeuze na kuhamishia kwenye shimo liliko pembeni. Kwa namna yoyote ile geuza rundo miezi miwili au mitatu kabla ya kupanda na uliache litulie ili kuiva, wakati huo ukianza kujaza shimo lile la kwanza.


Njia bora ya kuandaa mboji

2. Kutengeneza rundo • Andaa malighafi za kutengenezea mboji vizuri: Katakata malighafi za miti vipande vidogo vidogo ili ziweze kuoza. • Endapo malighafi unazotaka kutumia zimekauka, loweka kwanza kabla ya kuzichanganya. • Weka matabaka kwa kuweka fito chini ili kuruhusu maji yaliyozidi kupita kwa urahisi. • Panga safu za malighafi zilizokauka na mbichi kwa kutofautisha matabaka. • Weka samadi au mboji kwenye kila tabaka ili kuwezesha uozaji kirahisi. • Kama umechimba shimo jipya, ongeza udongo kidogo kidogo kwenye kila tabaka.

1. Kusanya malighafi Ili kufurahia faida zote za mbinu hii, kusanya malighafi zote kama vile mabaki ya jikoni na samadi inayotokana na mifugo mara kwa mara. Ni vizuri kuzikausha, kuzipooza na kuzifunika, kwa mfano kwa kutumia majani ya migomba au nyasi ili kuzuia upotevu wa maji kabla ya kutengeneza rundo la mboji. Udongo, mabaki ya mazao na mimea ya kijani inaweza kukusanywa siku ya kutengeneza rundo la mboji.

Malighafi zinazopendekezwa kuchanganywa Uozeshaji wa malighafi zilizokauka zinazotokana na mabaki ya mazao na miti huoza haraka zaidi zinapochanganywa na malighafi nyingine zinazo oza haraka kama vile mimea na kinyesi cha wanyama. Mchanganyiko unaopendekezwa ni: • Moja ya tatu ya nitrojeni-mali ghafi zenye nitrojeni kwa wingi, kama vile mimea mibichi, majani mabichi, magugu, mabaki ya jikoni,na samadi. Viumbe wadogo wanahitaji nitrojeni ili kuongezeka na kuweza kuvunja vunja malighafi hizo kuwa mbolea. • Moja ya tatu ya malighafi za kati ambazo zina kiasi kidogo cha nitrojeni (mabaki ya mazao yaliyokauka vizuri, majani yaliyokauka, mabua n.k) • Moja ya tatu ya rundo la malighafi zilizokatwa katwa kama vile matawi ya miti, magome ya miti, mabaki ya mazao. Malighafi hizi hukupa uhakika kuwa kuna hewa ya kutosha kwenye rundo la kutengenezea mboji.

• Unaweza kunyunyizia majivu ya kuni kwenye matabaka hayo ili kuongeza potashiamu. • Ukimaliza kutengeneza rundo, funika kwa kutumia nyasi kiasi cha sentimita 10, ili kuzuia kukauka.

3. Kugeuza na kufunika rundo la mbolea Baada ya wiki mbili mpaka tatu, joto linakuwa limepungua na rundo linakuwa limepungua ukubwa wake kwa kiasi cha nusu ya ukubwa wake wa awali. Huu ni muda muafaka wa kuligeuza. Unaweza kuligeuza mara mbili katika kipindi cha miezi miwili. Kugeuza rundo husaidia kuchochea uozaji, lakini si lazima endapo rundo lilitengenezwa vizuri na kuwa katika hali ya unyevu vizuri. Mboji inakuwa tayari baada ya miezi 2 mpaka 4 baada ya rundo kutengenezwa.

Ni nini tatizo la mboji yangu? Endapo mboji yako ikiwa na ukungu mweupe, hii ni dalili kuwa bakteria wamekuwepo kwa wingi kupita kawaida. Malighafi ni kavu sana na zimelegea legea. Kwa hali kama hii ina maana unatakiwa kuongeza maji na uchanganye na malighafi zenye madini ya nitrojeni kwa wingi (majani mabichi yenye kijani kwa wingi, mkojo, na samadi) na uhakikishe rundo hilo lipo katika hali ya unyevu. Kama malighafi zikiwa na rangi nyeusi-kijani na yana harufu mbaya, hii ni dalili kuwa malighafi hizo zina unyevu kupita kawaida na pia hazikupangwa vizuri. Sambaratisha rundo au ulipange tena vizuri, changanya maranda na malighafi nyingine zilizokauka kisha ulifunike kulikinga dhidi ya mvua.

Matumizi ya mboji

Mboji inaweza kutumika mara tu malighafi zilizotumika kutengenezea zinapokuwa zimeoza kiasi cha kutotambulika aina yake, kuwa nyeusi na harufu nzuri. Fito na nysi nene huwa haziozi kabisa, na zinaweza kuonekana. Hatua hii inapofikiwa, inategemeana na malighafi zilizotumika, hali joto ya nje, na kiasi cha unyevu kilichopo kwenye rundo. Hii inaweza kuchukua muda wa miezi mitatu au minne baada ya kugeuza rundo la mboji. Mboji ambayo haikuiva ipasavyo inaweza kusambazwa shambani kama matandazo, wakati iliyoiva vizuri inaweza kutumika inavyotakiwa.

kuboresha udongo. Kwa kawaida ni vigumu kuzalisha mboji ya kutosha kurutubisha shamba lote. Hivyo basi ni muhimu kuwekwa sehemu ambayo inaonekana kuwa na faida zaidi:

Ni vizuri kuweka mboji karibu na ukanda wa mizizi ya mmea. Weka kiganja kimoja kwenye kila shimo kabla au wakati wa kupanda.

• Kwenye vitalu vya miti

Endapo una andaa kitalu kwa ajili ya kuoteshea miche, tumia mabeleshi mawili yaliyo jaa na uyasambaze kwenye eneo la kitalu, iwe na unene wa sentimita 1. Mboji ni bidhaa hadimu na yenye thamani sana katika

• Kwenye sehemu ya kusia mbegu • Kwenye mashimo ya kupandia Kwa ajili ya kufahamu virutubisho vinavyopatikana kwenye mboji, tafadhali soma moduli ya MkM namba 4 (Virutubisho vya mazao ya kilimo hai)


Mbolea ya mifugo

Mbolea inayotokana na mifugo ni mbolea muhimu na yenye thamani katika shughuli za kilimo na imetumika kwa karne nyingi kuboresha rutuba katika udongo na uzalishaji wa mazao. Ni moja ya vyanzo vizuri vya nitrojeni (N) katika kilimo hai, na pia inatoa fosiforasi (P) na potashiamu (K). Kwa sababu kuna athari zinazoambatana na matumizi ya samadi ni vizuri ukaozesha kwanza kabla ya kuitumia shambani. Kuozesha kinyesi cha mifugo ni njia nzuri zaidi ya utunzaji na matumizi kwa mkulima mdogo.

Faida za samadi iliyo ozeshwa • Samadi iliyooza ina virutubisho vya hali ya juu kuliko iliyokauka kwa sababu upotevu unakuwa ni mdogo sana • Kuozesha kunasaidia kuondoa vimelea vya magonjwa pamoja na mbegu za magugu • Inapunguza uwezekano wa vimelea kuwaathiri mifugo wako, hii ni kwa sababu joto linalokuwepo kwenye mboji wakati wa kuoza huua mayai ya vimelea • Mboji huchangia kwa kiasi kikubwa virutubisho vya asili kwenye udongo kuliko samadi • Haiana harufu kali, na ni nzuri zaidi kutumia,ni laini kuliko samadi • Hatua ya kuvundika husaidia kuoza haraka kwa rundo la mboji Kufahamu virutubisho mbalimbali vinavyopatikana kwenye samadi, soma moduli ya MkM-namba 4 (Virutubisho vya mazao ya kilimo hai).

Kuwa makini na mbolea mbichi inayotokana na mifugo Samadi ina kiasi kikubwa cha virutubisho vya nitrojeni (N) vilivyoyeyuka. Lakini kulingana na kiasi kikubwa cha ammonia, inaweza kuunguza mazao. Mbolea mbichi pia huwa na kiasi kikubwa cha vimelea kama vile E.coli (bacteria). Hivyo, ni lazima kuchukua tahadhari unapotumia mbolea mbichi katika mazao ya chakula. • Samadi ni lazima itumike kwa kiwango cha kati. • Ili kuepuka upotevu wa virutubisho kutoka kwenye aina hii ya mbolea ambayo ni hadimu, tumia wakati ardhi ikiwa na unyevu, na uwe mwangalifu. • Ni lazima kuwepo na kipindi cha miezi minne toka ulipoweka samadi shambani mpaka wakati wa kuvuna mazao ambayo ni kwa matumizi ya binadamu.

Mbolea Maji

Mbolea maji, hutoa virutubisho vya haraka sana wakati wa ukuaji. Ni rahisi na yenye virutubisho vingi vya nitrojeni na mbolea ya asili ambayo hutumika zaidi kwa ajili ya mboga mboga kwa kunyunyizia. Inaweza kutengenezwa kutokana na samadi au kutokana na mimea.

Mbolea maji ya samadi • Jaza samadi kwenye kiroba cha kilo 50 au aina nyingine ya mfuko wenye matundu, funga vizuri, kisha utumbukize kwenye maji robo tatu ya dramu. • Weka mfuniko au karatasi ya nailoni ili kuzuia upotevu wa nitrojeni. • Koroga kwa kunyanyua mfuko huo juu na kuurudisha kila baada ya siku tatu. • Baada ya wiki 2 mpaka 3, virutubisho vitakuwa vimeyeyuka kwenye maji. Harufu haitakuwa mbaya sana, lakini mbolea itakuwa na ufanisi mkubwa.

Mbolea maji inayotokana na mimea Aina zote za mimea inayokuwa vizuri inaweza kutumika, ikiwa ni pamoja na magugu na nyasi. Tumia shina laini na majani machanga au mimea ambayo bado inakuwa. Mimea ambayo ni mizuri zaidi ni ile milaini kama vile alizeti pori (tithonia). Jaza kiroba na mimea iliyokatwa katwa vizuri, kisha ufuate hatua sawa na zile za kutengeneza mbolea maji inayotokana na samadi.

Matumizi • Changanya mchanganyiko huwa mpaka uwe mwepesi na rangi ya kahawia.

• Tumia mara mbili au tatu kwa wiki kunyeshea mimea.

• Kuwa mwangalifu usimwagilie mbolea maji ya samadi juu ya majani ya mmea wowote ambao utaliwa.

• Mbolea iliyotengenezwa kutokana na mimea inaweza kutumika kwa kunyunyizia. Isiwe nzito sana. Changanya mchanganyiko huo mpaka uwe mwepesi na kahawia ambayo haijakakolea. Moduli hii imechapishwa na Mkulima Mbunifu kwa ushirikiano na The Organic Farmer (info@organickenya.org, P.O. Box 14352-00800 Nairobi, Kenya, +254 20 440398), Biovision Africa Trust, www.biovision.ch

Imeandaliwa na Theres SZekely na kutafsiriwa na Ayubu Nnko Mkulima Mbunifu: S.L.P. 14402 Makongoro Street Arusha Rununu: 0717 266 007, 0785 133 005 www.mkulimambunifu.org Barua pepe: info@mkulimambunifu.org


Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.