Moduli 6, Mbulea vunde, mimea inayotambaa, matandazo, palizi (revised)

Page 1

Mkulima Mbunifu Moduli namba 6

MBOLEA VUNDE, MIMEA INAYOTAMBAA, MATANDAZO, PALIZI Boresha rutuba kwenye udongo na upunguze magugu! Mbolea vunde, mimea inayotambaa na matandazo ni moja ya njia muhimu sana za kuongeza rutuba kwenye ardhi inayotumika kwa kilimo. Wakati huo huo inafunika udongo na kuzuia mmomonyoko wa ardhi. Udongo ukifunikwa vizuri huzuia magugu na hivyo kupunguza usumbufu wa kukabiliana na magugu.

Mbolea vunde

Kutumia mbolea vunde kwa ajili ya kurutubisha udongo badala ya kutumia mbolea za viwandani ni mbinu bora ya asili. Mimea inayotumika kama mbolea vunde hupandwa kabla ya zao la msimu. Kwa kawaida hufyekwa wiki mbili au tatu kabla ya kupanda zao la msimu, kabla au wakati inachanua, wakati ambao inakuwa imekusanya nitrojeni kwa wingi. Inawekwa juu ya udongo ili ioze na kulisha mazao kwa virutubisho iliyobeba (Pichani: Muonekano wa Clotalaria) Hata hivyo mimea mibichi kama vichaka na matawi ya miti inaweza kutandazwa shambani wiki moja au mbili kabla ya kupanda.

Faida za mbolea vunde •

Kiasi kikubwa cha malighafi zinazo oza huongezeka kwenye udongo, na kuhamasisha viumbe hai waliomo kwenye udongo.

Mbolea vunde huoza kwa urahisi na kutoa virutubisho haraka, hii ni kwa sababu ni laini katika hatua za mwanzo za ukuaji.

• Mimea jamii ya mikunde hupata nitrojeni kutoka kwenye hewa na kuhifadhi kwenye mimea. Nusu ya nitrojeni hiyo itapatikana kwa ajili ya mazao, na wakati mwingine virutubisho hivyo hupatikana kwa zao litakalofuata kupandwa kwenye eneo hilo hilo. Kwa mfano, Kawa ya zambarao (Purple vetch) inaweza kukusanya kilo 90 za nitrojeni kwa heka moja na inaweza kutoa kiasi cha kilo 45 za nitrojeni kwa ekari moja ya mazao ya nafaka au mboga mboga.

Mimea inayotambaa Mimea inayotambaa inalimwa ili kufunika udongo, kuweka mbolea asili, na kupunguza magugu.

Inaweza kuwekwa shambani inapokuwa michanga au kutumika kama matandazo hasa inapokuwa imekomaa. Mimea inayotambaa hutumika kufunika ardhi wakati wa kiangazi au wakati wa baridi, na huzungushwa tu au kufyekwa na kuachwa shambani wiki moja au mbili kabla ya kupanda zao la msimu.

Mimea jamii ya mikunde inapendekezwa kutumika zaidi kwa kusudio hilo, na hata hivyo jamii ya mimea mingine kama hiyo hutumika kwa kama mbolea vunde. Mimea inayotambaa hutoa malisho kwa ajili ya mifugo na mara nyingine chakula kwa ajili ya matumizi ya binadamu kama vile maharage au kunde(Pichani: Kunde ikiwa imepandwa kama mimea inayotambaa kwenye shamba la mtama)

Matandazo

Matandazo ni tabaka la malighafi zozote, kwa kawaida zinazotokana na mimea, zinazotandazwa ardhini. Tabaka la taka zinazooza hujenga hali zote za mazingira ya asili-jangwani haina ufanisi!

Matandazo huifadhi unyevu kwenye udongo, kuweka uwiano wa joto kwenye ardhi, na hutoa virutubisho vya asili kwenye udongo yanapo oza. Matandazo hufanya mimea dhaifu na laini kama vile strawberries(Pichani) kuwa imara na kuonekana safi.

Matandazo yanaweza kutumika duniani kote. Malighafi changa, na laini huoza kwa haraka sana na hivyo kutoa virutubisho kwenye mimea ndani ya kipindi kifupi, wakati inapooza taratibu, malighafi zilizo komaa, hulinda udongo kwa muda mrefu.

Matandazo ya plastiki hufanywa kwa kutumia nailoni nyepesi kufunika udongo. Mimea hupandwa kupitia matundu kwenye karatasi hiyo na hunyeshewa kwa njia ya matone. Hata hivyo, upatikanaji wa nailoni hizo ni tatizo.

Hizi ndizo faida za mbinu zote tatu • Zinafunika udongo na kupunguza mmomonyoko wa ardhi. • Zinazuia magugu kuota na kuyapunguza. • Zinatengeneza virutubisho vya asili kwenye udongo, na kuboresha muundo wa udongo, na kuongeza uwezo wa udongo kuhifadhi maji na rutuba.

• Zinaboresha afya ya mazao kwa ujumla pamoja na mavuno. • Zinatoa virutubisho kwa aina nyingine za mazao. • Mimea yenye mizizi mirefu inaweza kukusanya na kurudisha virutubisho kwenye mzunguko kutoka tabaka la chini la udongo. • Ni rahisi na zenye ufanisi katika kufufua na kuboresha udongo.


Mbolea vunde na mimea itambaayo jamii ya mikunde kwa Tanzania Aiana nyingi za mimea jamii ya mikunde zimefanyiwa utafiti kwa muda mrefu na kuonekana kuwa zinafaa kutumika kama mbolea vunde, na mimea inayotambaa. Baadhi ya mimea hiyo imekuwa ikichukuliwa kama yenye faida zaidi. Lakini mbali na ukweli huo, wakulima wengi wamekuwa hawalimi mazao ambayo hayaliwi. Mbegu zimekuwa ni tatizo kwa wakulima ambao wanahitaji kujaribu. Orodha hii iliyopo hapo chini haijakamilika, unaweza kuwauliza maafisa kilimo waliomo katika eneo lako aina inayopatikana!

Njegere/ Mbaazi (Pigeon pea, cajanus cajana) Mbaazi zinafaa zaidi kwa kilimo mseto.

Mbaazi zinafaa zaidi kwa kilimo mseto. Hazishindani na mazao mengine kwa kuwa zina mizizi inayoenda chini sana na pia hukua taratibu. Zinafaa sana kwa sehemu kame na pia sehemu ambayo udongo una rutuba hafifu. Mabaki yake baada ya mavuno yanaweza kutumika kama matandazo shambani kabla ya kupanda tena. • Mseto: Na mahindi, mtama, ulezi, pamba, karanga, mihogo, na mengineyo. Baada ya kuvuna zao la msimu, njegere huendelea kukua ili kulinda udongo (Pichani) • Mseto na nyasi: Njegere huongeza ukuaji wa nyasi. • Sole stand: Panda sole kwenye mzunguko ili kuboresha udongo na kuuwezesha kuzalisha zaidi.

Lablab Lablab ina afya na inastahimili ukame. Inatoa malisho mazuri sana kwa mifugo,

na majani yake yanaweza kuandaliwa na kutumika kama mboga. Viriba vyake hukomaa baada ya miezi mitano, na uvunaji unaweza kuendelea kwa kipindi cha miezi 6. Lablab hukatwa na kuachwa shambani kama matandazo kabla ya kupanda zao la msimu. • Inaweza kupandwa mseto na mahindi: Panda mbegu 2 kwa kila shimo kila baada ya sentimita 60 katikati ya mistari ya mahindi, inapendekezwa iwe wiki 3-4 baada ya kupanda mahindi ili kuepuka ushindani. • Mimea yenye tija (Pure stand): Kwenye mzunguko mimea yenye tija ina faida kwa udongo. Kwenye udongo hafifu, lablab itafaa sana kama samadi itawekwa pia.

Mucuna Mucuna hukua kwa haraka sana na huimarisha na kuboresha rutuba ya udongo na uzalishaji kwa ujumla. Mucuna inaweza kuliwa na wanyama wanaocheua peke yake na ni sumu kwa binadamu. Kutumia kama malisho, kata mucuna kabla haujachanua na ukiwa na urefu wa sentimita 40 kwa ukuaji wa haraka. Lisha ikiwa mbichi, lakini kiasi kikubwa kiwe 20% ya resheni ya malisho. • Panda mseto na mahindi: Panda mucuna baada ya wiki 3-4 baada ya kupanda mahindi kwa kuwa zina ushindani mkubwa na mazao mengine. Panda mbegu moja kila shimo katikati ya mistari ya mahindi umbali wa sentimita 50. Acha mucuna iendelee kukua wakati wa kiangazi. Jumuisha au ng’oa kisha uache shambani kabla ya kupanda zao la msimu linalofuata. • Panda mseto na migomba: Panda mbegu moja ya mucuna katikati ya migomba minne. Ni lazima kukata mucuna mara kwa mara ili kuepusha usipa nde kwenye migomba. • Zao moja: Mucuna huonesha matokeo mazuri sana katika kufifisha magugu. Huongeza mavuno kwa misimu mawili yatakayofuata, na huboresha udongo uliodhoofika (Tazama Pichani). Clotalaria (Sun hemp) Clotalaria inakuwa

• • •

haraka na hukomaa katika kipindi cha miezi 3-4, hustahimili ukame na kustawi katika ardhi yenye rutuba hafifu. Ina uwezo wa kuongeza kiwango cha nitrojeni ardhini kwa ufanisi mkubwa. Baadhi ya aina inaweza kuliwa wakati aina nyingine ni sumu. Lisha mifugo yako kwa kiwango cha 10% ya resheni ya malisho. Panda mseto na mahindi: Panda kiasi cha mbegu 100 kwa mita moja katikati ya mistari ya mahindi, wiki 3 baada ya kupanda mahindi. Acha ikue na usisahau kuvuna mbegu, kisha ng’oa na kutandaza shambani muda mfupi kabla ya kupanda zao la msimu. Panda mseto na mihogo: Panda mistari miwili ya clotalaria katikati ya mistari mara baada ya kupanda mihogo. Mazao mengine: Viazi vitamu, migomba, kahawa, na mazao mengine. Epuka kupanda clotalaria karibu sana na mazao hayo. Zao moja: Kuboresha uwezo wa ardhi, panda clotalaria wakati wa mvua za muda mfupi (Vuli).

Canavalia

(Jackbean)

Canavalia inaboresha udongo uliochoka na huvumilia ukame na kivuli. Ni rahisi kutunza na inaweza kupandwa mseto na aina zote za mazao. Inaweza kupandwa wakati wa kiangazi. Baada ya kuvuna viriba kwa ajili ya kuhifadhi mbegu, mabaki huachwa shambani kama matandazo. Canavalia inaweza kutumika kama malisho ya mifugo, lakini ni lazima inyaushwe baada ya kukatwa na kulishwa kwa kiwango kidogo sana kwa kuwa ina viini vyenye sumu. • Panda mseto na mahindi: Panda canavalia wiki 4 baada ya kupanda mahindi. Panda mbegu moja kwenye kila shimo katikati ya mistari ya mahindi, kila baada ya sentimita 50, kama ilivyo kwa mucuna (Tazama picha). • Panda mseto na migomba au kahawa: Panda mistari miwili yenye sentimita 60 katikati ya mistari ya kahawa au migomba. Weka umbali wa mita moja kutoka kwenye mgomba au kahawa. Itumie kama matandazo. • Panda mseto na viazi vitamu: Panda canavalia kwenye mistari. Baada ya kuvuna viazi vitamu, jumuisha canavalia au uiche kama matandazo shambani. • Zao moja: Kwenye shamba ambalo lina kiasi kidogo cha rutuba, panda mbegu moja kila baada ya sentimita 30 kwenye mistari yenye nafasi ya sentimita 75. Mwisho wa msimu, vuna viriba na uiache shambani kama matandazo.


Mambo ya kuzingatia • Kama mabaki ya mazao au mimea inayotambaa ikiachwa shambani huoza taratibu na virutubisho huachiliwa kuingia kwenye ardhi taratibu. Udongo unakuwa umefunikwa hivyo kulindwa kwa muda mrefu jambo ambalo ni la faida. • Magonjwa na wadudu wanaweza kuishi kwenye mabaki ya mazao. Kuepuka kuendelea kuwepo ni vizuri kufanya kilimo cha mzunguko. • Kuozesha kiasi kikubwa cha malighafi ngumu kama miti au mabua, viumbe hai wadogo waliopo ardhini wanahitaji nitrojeni ambayo kwa muda fulani haitapatikana kwa ajili ya ukuaji wa mimea. Inaweza kuwa na faida zaidi kuongeza nitrojeni kama unaona kama mimea ina ukosefu wake kutokana na matandazo. • Mbolea vunde inapowekwa shambani kabla ya kupanda inasaidia uwepo wa viumbe hao wanaohitajika kwenye udongo. Wadudu hawa huwa wanasaidia kuvunja vunja malighafi laini na hivyo kufanya virutubisho kupatikana kwa wingi. Vitalu vidogo havina uwezo wa kuvipata vyote, na hii hutokana na virutubisho kuzama ardhini kupitia maji. Kwa kuongezea, kuna hatari ya kuwepo mmomonyoko wa ardhi kwa kuwa udongo unakuwa haujafunikwa na mimea wala matandazo wakati wa kuimarisha kitalu. • Kama mazao jamii ya mimea inapandwa sehemu kwa mara ya kwanza, kuchanganya mbegu na bakteria aina ya Rhizobia inaweza kuwa lazima ili kuwezesha upatikanaji wa nitrojeni. Bakteria hao wanaweza kupatikana kutoka kwa wauzaji wa mbegu.

Baadhi ya mifumo iliyozoeleka Mbolea ya kijani kama zao moja wapo la kuboresha rutuba kwenye udongo Kwenye baadhi ya maeneo ambayo mvua za pili siyo za kutegemea au mara nyingine kunyesha kwa muda mfupi, panda mahindi kama zao la msimu mvua inaponyesha kwa muda mrefu. Baada ya kuvuna mahindi panda mimea inayotengeneza mbolea vunde hasa jamii ya mikunde na uiache shambani mwako muda wote wa kiangazi. Fyeka na uichanganye shambani wakati wa maandalizi ya shamba kabla ya msimu mwingine wa mvua za muda mrefu.

Panda mseto wa mimea jamii ya mikunde na mahindi Kwenye ukanda wenye misimu miwili ya mvua za muda mrefu kwa mwaka, mimea ya mbolea vunde kwa kawaida hupandwa wakati mmoja na mahindi. Mimea inayokuwa haraka kama vile mucuna na lablab ipandwe wiki 2 mpaka 4 ili kulipa faida zao la msimu. Fanya palizi kama ni lazima. Mimea jamii ya mikunde hupandwa katikati ya mistari ya mahindi na kuachwa ikikua wakati wa kiangazi. Hufyekwa na kujumuishwa kwenye udongo mwanzo wa msimu wa mvua. Kwenye ukanda wenye msimu mmoja tu wa mvua za muda mrefu kwa mwaka, mimea jamii ya mikunde inayotambaa hupandwa mwezi Agosti, miezi minne baada ya kupanda mahindi (Hii inategemea na ukanda uliopo). Majani ya chini ya mahindi hukatwa (ni chakula kizuri cha ng’ombe wa maziwa) ili kuruhusu mimea jamii ya mikunde kujiimarisha vizuri. Mikunde hiyo hufyekwa na kujumuishwa kwenye udongo wiki 2-3 kabla ya kupanda zao linalofuata msimu huo.

Kupanda mseto wa mimea vunde na mboga mboga Mikunde inaweza kupandwa mseto na badhi ya mboga kama vile Kale. Chagua aina ya mikunde ambayo inakuwa kwenda juu na haitajizungusha kwenye mboga, mf.crotalaria au ngwara.

Mbolea vunde kutokana na vichaka na miti Alizeti mwitu ni moja ya mimea inayotengeneza mbolea vunde yenye ufanisi wahali ya juu kwa kuwa huoza haraka na huota katika maeneo mengi nchini Tanzania (Tazama picha hapo juu). Kata ikiwa changa kabla haijaanza kuchanua na uichanganye kwenye udongo (kilo 3 mpaka 5 kwa skwea mita )wiki 1-2 kabla ya kupanda mboga.

Mbolea vunde yenye tija kwa udongo Mimea inayotengeneza mbolea vunde hufanya kazi vizuri zaidi inapokuwa bado michanga na mibichi. Inashauriwa kukata kata ili ioze kwa urahisi zaidi. Mimea inapokuwa imekomaa ndivyo huchukua muda mrefu zaidi kuoza.

Mimea itambaayo kwenye mashamba makubwa Kwenye mashamba makubwa( kahawa, chai, minazi, miwa n.k) mimea itambaayo husaidia kwa kiasi kikubwa kufifisha magugu, kudhibiti mmomonyoko na kuweka ardhi katika hali nzuri ya kukuza mazao.

Uhifadhi kwenye kilimo kwa kutumia matandazo Mimea inayotambaa ni muhimili muhimu kwenye uhifadhi wa kilimo. Hata katika ukanda wenye ukame, mimea inayotambaa kama vile lablab inaweza kutumika kufunika ardhi katika kipindi chenye ukame mkali zaidi. Mimea jamii ya mikunde huachwa shambani kufunika udongo, na zao lingine kupandwa moja kwa moja juu ya tabaka la matandazo hayo.

Matandazo kwenye mazao yenye ubora wa juu Matandazo kwa kawaida huwekewa mimea michanga hasa kwa upande wa mbogamboga ili kuhifadhi unyevu kwenye udongo na kufanya udongo kuwa na hali ya hewa nzuri. Matandazo huwekwa kwa kutumia mikono au reki, linakuwa na unene wa inchi 1 mpaka 4. Kwenye eneo lenye unyevu kwa wingi, matandazo yenye tabaka jembamba linatakiwa wakati sehemu kame tabaka nene linahitajika. Mimea mibichi ni lazima iachwe ikauke au inyaushwe kabla ya kutumika kama matandazo.

Tithonia hutoa matandazo mazuri sana-na virutubisho Sehemu ambayo alizeti mwitu (Tithonia) imetumika kama matandazo mimea huonesha ukuaji wa haraka. Panda alizeti mwitu kwenye uzio kuzunguka shamba lako! Unaweza kukata mara kadhaa katika kipindi cha mwaka, kiasi cha kuwa na urefu usawa wa magoti. Kata shina kabla hazijaanza kuchanua, na zinapokuwa na urefu wa mita 2. Kata na utandaze kiashi cha inchi mbili kuzunguka kila shina shambani.

Matandazo kwenye migomba Matandazo ni lazima yawekwe umbali wa sentimita 60-90 kutoka kwenye shimo la mgomba, ili kuruhusu ukuaji wa maotea. Matandazo yanapowekwa karibu na shina la mgomba husababisha uwepo wa mizizi mingi zaidi inayotambaa kwenye tabaka la juu la udongo. Mmea utakuwa na hali mbaya wakati wa kiangazi, na pia kuna uwezekano wa mgomba kung’olewa na upepo mkali.


Njia za asili za kudhibiti magugu Tabaka lote la juu la udongo lina kiasi kikubwa cha mbegu za magugukuna usemi kuwa mbegu hizo zinatosha kwa mamia ya miaka. Kila wakati udongo unapohamishwa, nyingi zaidi huota. Magugu ni lazima yadhibitiwe, vinginevyo yatachukua nafasi hiyo kuchukua na kunyonya virutubisho muhimu kutoka kwenye mbolea na kwenye udongo na kuiacha mimea yako ikiwa dhaifu na yenye njaa. Mkulima anaefanya kilimo hai, huwa hatumii dawa za viwandani kukabiliana na magugu kwa sababu baadhi zinaweza kuwa na madhara kwa binadamu na mazingira. Baadhi ya kemikali hizo hukaa kwenye udongo kwa muda mrefu, na zinaweza kuchafua maji yaliyopo kwenye uso wa dunia na hata chini ya ardhi. Kwa mantiki hiyo mkulima anaefanya kilimo hai, hutegemea zaidi kulima kwa mzunguko, kupalilia kwa mikono, na kufunika udongo kwa matandazo. • Fanya mzunguko wa mazao. Mzunguko wa mazao huepusha aina fulani ya magugu kutawala sehemu ya shamba lako. • Panda mimea inayotamba na kufunika ardhi kama vile maharage, lablab, desmodium, mucuna n.k. Kwa kawaida kufanya palizi mara moja ni muhimu ili kuwa na uhakika wa uimara wa mimea inayotambaa. Baada ya hapo, magugu yatakayo ota tena ni lazima yadhoofishwe.

Mikunde ni muhimu sana kwa kuwa hutoa nitrojeni yake yenyewe. Hii huachwa ikiendelea kukua baada ya kuvuna zao kuu, hii husaidia kuendelea kulinda udongo mpaka zao linalofuata litakapopandwa. Mikunde inaweza kutumika kwa malisho ya mifugo, au kama mbolea vunde, au kama matandazo kwa ajili ya zao la msimu litakalofuata.

• Weka matandazo kwa kuacha tabaka la mabaki ya mazao au mimea mingineyo shambani. Mbali na kudhoofisha magugu, pia husaida kupooza udongo, kuhifadhi unyevu, kuzuia udongo kukauka, na kuongeza malighafi zinazooza na kuweka virutubisho kwenye udongo. • Fyeka magugu kabla ya kupanda. Hatua hii huruhusu mwanzo mzuri wa maendeleo ya mazao. • Wakati wote fanya palizi mapema kabla magugu hayajaanza kushindana na mazao na kuchukua virutubisho vyote! • Fyeka magugu yawe kweye usawa wa ardhi yanapokuwa na urefu wa sentimita 10-15, na kabla hayajaanza kuchanua na kutoa mbegu, kisha yaache shambani kama matandazo. Hii husaidia kupunguza kazi ya palizi, na uondoaji wa magugu unaweza kufanyika kwa njia za asili kama vile kutumia jembe la mkono.

Epuka kufanya haya! • Kuondoa magugu shambani ina maanisha kuwa utaondoa pia virutubisho vyote ambavyo vilikusanywa na magugu hayo. Yaache shambani kama matandazo au weka kwenye mzunguko wa mbolea. • Ardhi iliyo wazi isiyofunikwa ni rahisi zaidi kumomonyolewa na mvua, pia kukaushwa na jua. Kuacha udongo wazi ni kufanya uharibiwe kirahisi zaidi. • Kufanyia shamba lako usafi kwa kuchoma, siyo kwamba inaondoa tu magugu na mabaki ya mazao, lakini pia malighafi za asili zinazooza zilizopo kwenye tabaka la juu la udongo. Hali hii haitaboresha wala kujenga rutuba kwenye udongo, lakini hupunguza na kuiharibu kwa kipindi kifupi sana. Magugu jamii ya mikunde yakitumika hasa yenye majani matatu, husaidia kuboresha rutuba kwenye udongo. Hii hutumika kufunika tabaka la ardhi na huzuia magugu kuota na mmomonyoko, mf. Kwenye shamba la karakara (passion). Mikunde inapokuwa kwa haraka, inaweza kukatwa na kutumika kwa malisho au kama matandazo kwenye mazao mengine.

Udhibiti wa magugu kwenye mazao yanayopandwa kwa mstari

Sangare-Sedge (Hizi hujumuisha pia magugu maji) aina hii ya mimea hutoa aina fulani ya kimikali ambayo hupunguza ukuaji wa mimea mingine iliyo karibu yake. Hata mazao pia hukua kwa shida sana sehemu ambayo kuna sangare (sedges). Aina hii ya mimea ina mizizi inayokwenda chini sana kiasi kwamba hata baada ya palizi mizizi inayobaki ardhini huota tena.

Hakikisha udongo umefunikwa kwa kutumia mimea sahihi wakati wote wa msimu. Mimea jamii ya mikunde inayopandwa mseto na mahindi au mihogo ipandwe moja kwa moja mara tu baada ya palizi ya kwanza. Jamii ya mikunde isiyokuwa kwenda juu inafaa zaidi kufanya mseto na nafaka ndogo pia. Njegere huboresha udongo na kufanya mavuno ya zao ilipochanganywa kuwa mazuri na bora, wakati husaidia pia kudhibiti magugu.

Witchweed (Striga) magugu haya hukua vizuri katika sehemu kame. Ili kuboresha rutuba kwenye udongo unahitajika kudhibiti striga: Tumia mboji na samadi, fanya kilimo mzunguko na mseto na uboreshe mazao yako kwa kutumia mimea jamii ya mikunde pamoja na mimea inayotambaa, na pia matandazo kwa kutumia mabaki ya mazao shambani.

Mabaki ya mazao baada ya mavuno na mimea inayotambaa iachwe shambani kwa kipindi chote cha kiangazi ili kulinda udongo. Kwenye sehemu yenye mwinuko isiyokuwa na kontua, acha mabua shambani kwa mchazari ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Alizeti mwitu (Tithonia) Hii haitakiwi kuchukuliwa kama magugu! hutoa mbolea yenye nitrojeni kwa wingi majani yake yanapodondoka au kutumika kama matandazo (Tazama ukurasa uliopita)

Moduli hii imechapishwa na Mkulima Mbunifu kwa ushirikiano na The Organic Farmer (info@organickenya.org, P.O. Box 14352-00800 Nairobi, Kenya, +254 20 440398), Biovision Africa Trust, www.biovision.ch

Imeandaliwa na Theres SZekely na kutafsiriwa na Ayubu Nnko Mkulima Mbunifu: S.L.P. 14402 Makongoro Street Arusha Rununu: 0717 266 007, 0785 133 005 www.mkulimambunifu.org Barua pepe: info@mkulimambunifu.org


Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.