Mwongozo wa Siku ya Maombi kwa ajili ya watoto wa ulimwenguni 2010 Mtoto katikati yetu Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki. Marko 10: 16 Mungu Baba, tunakuja kwako leo tukikuomba kwa pamoja kwamba uguse maisha ya watoto ambao hawajapokea mikono ya upendo wala mahali pa kuishi salama. Tunasikitika, kwa sababu hata sisi tumekosa mara nyingi moyo na mikono ya kuwapokea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili tuwahudumie na kuwaonesha mapenzi yako kwa ulimwengu huu. Tunakuomba kwamba, vilio vya watoto hawa wanaoteseka kwa sababu ya mazingira hatarishi visikike na wale wanaoliamini Jina la Yesu Kristo. Tunakuomba uwatume wavunaji zaidi katika shamba lako la mamilioni ya watoto hawa. Tunakuomba uwalete watetezi wengi zaidi, Baba na Mama wanaoshuhudia upendo wako katika ulimwengu huu wenye tabu. Tunakuomba kwamba jamii zibadilike na watoto waweze kuona upendo wako, na ulimwengu utajua habari njema ya ufalme wako ikiwa watu wanafanya kazi kwa pamoja katika upendo na umoja. Amina. Mwongozo huu wa siku ya maombi kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi umeandaliwa juu ya msingi wa wazo la kumweka mtoto katikati yetu. Kila sehemu ya mwongozo unamtambulisha mtoto mmoja aliyeteseka kwa njia moja ama nyingine na inatutia moyo tumwombee pamoja na hali hii yote. Kwa watoto wengi dunia yetu inaweza kuonekana kuwa imeharibika na kukosa matumaini – lakini sisi tunaamini na kujua kwamba tumaini lipo! Kwa hiyo tunapenda kuongezeka idadi ya wakristo wanaoshiriki na kuomba kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ulimwenguni kote. ’Waacheni watoto waje kwangu’ Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwagusa, lakini wanafunzi wakawafukuza. Yesu alipoona hayo, alikasirika na kuwakemea wasifanye hivyo. Aliwaambia: ”Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo.“ Marko 10: 13-15