Biblia ya YesKids Hadithi na Maombi - Kiswahili

Page 1

Biblia hii inayovutia yenye vielelezo vya rangi iitwayo Yeskids imeandaliwa maalumu kwa watoto wa Yeskids! Kila hadithi imefuatiliwa na maombi kumsaidia mtoto aunganishwe na Mungu; kithaminisho cha Kikristo na mchezo wa kubahatisha ambao unakazia hiyo hadithi. Kitabu hiki kitawasaidia watoto wawe Yeskids. Mtoto wa Yeskids husema Ndiyo kuu! Katika kumfuata Yesu na katika kuishi maisha mema na ya furaha.

Mwongozo kwa wazazi: YesKids kimeandaliwa kwa kuzingatia hatua za kukua za mtoto wako na silka yake ya kipekee. Kinasaidia katika kujenga imani, maneno ya kuongea, na hata ujuzi wa kusoma na maendeleo ya kihisia. Kwa maelezo kamili ya alama fungua ukurasa wa 108 hadi 109.

Hatua za maendeleo

Silka za kipekee

Kujenga imani

Msamiati

Usemi

Ujuzi wa kusoma

Ujuzi wa kusikiliza

Mapendekezo namna ya kufurahia kitabu hiki na mtoto wako: • Someni hadithi ya Biblia, • Ongeeni juu ya hadithi na Vithaminisho vya Kikristo wewe pamoja na mtoto wako, • Chezeni mchezo wa kubahatisha na • Tamkeni maombi kwa pamoja.

Kwa kadri wewe na mtoto wako mnavyokuwa karibu na Mungu, ndivyo hivyo mtakuwa karibu kila mmoja kwa mwenzake.

The YesKids Bible – Stories and Prayers (kiSwahili)

ISBN: 978-0-10920-592-4

www.christianmediapublishing.com



Kwa mtoto wangu: _________________________ Kwa upendo toka kwa: ______________________



Biblia ya

-H

iadithi na Maomb


Angalizo kwa wazazi Tunatumaini kwamba mtafurahia kusoma na kusikiliza hadithi hizi pamoja na mtoto wako. Kuna njia kadhaa mnazoweza kuzifurahia katika Biblia hii kwa pamoja: • Mnaweza kusoma hadithi hizi kwa sauti kubwa kwanza na kisha mcheze mchezo wa kubahatisha pamoja na mtoto wako. • Mara mtoto wako atakapokuwa amezoea hadithi hizo unaweza kufuatilia kwenye kitabu huku mkicheza mchezo wa kubahatisha. Hadithi hizi za Biblia zimesimuliwa tena kwa maneno ambayo watoto wadogo wanaweza kuelewa kwa urahisi, lakini huku zikiwa zimetunza kwa uaminifu ujumbe wa maandiko. Katika kitabu chote kizima, kusudi letu limekuwa ni kuwasaidia watoto kujenga uhusiano wa upendo na wenye nguvu pamoja na Mungu. Maneno na picha zinasisitiza zaidi vithaminisho vya kibiblia. Unaweza kutumia picha kusisimua mazungumzo kuhusu Mungu na Imani. Katika kila mwisho wa hadithi utakuta maombi ya kuomba na kithaminisho au ujumbe wa kumshirikisha mtoto wako. Angalia kwenye wanyama rafiki wanaoonekana katika hadithi za biblia, mmoja wapo wa hao wanyama atamsaidia mtoto kukumbuka ujumbe au kithaminisho cha hadithi. Mnyama mwingine anatoa kielelezo cha mchezo wa kubahatisha ambao unafuatana na kila hadithi. Kitabu hiki cha hadithi za Biblia ni zaidi ya kitabu cha hadithi. Kitumie kuwafundishia watoto furaha na maana ya kuwa Mkristo, na kile ambacho Yesu anaweza kumaanisha katika maisha yao.

6


Yaliyomo 1. Mungu wangu ni Mkuu sana! 2. Daima msikilize Mungu! 3. Hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu! 4. Mungu amfanya punda aongee! 5. Mungu husikia maombi yako 6. Nena Bwana, ninasikiliza! 7. Solomoni, Mfalme mwenye hekima 8. Mungu anatoa chakula na maji 9. Mungu ana nguvu kuliko Baali 10. Nehemia asaidia kuipendezesha tena Yerusalemu 11. Kwa msaada wa Mungu 12. Danieli katika pango la simba 13. Yona akataa kumtii Mungu 14. Yesu amezaliwa 15. Yesu anatembelea Hekalu 16. Mikate mitano na samaki wawili 17. Hakuna mwingine kama Yesu 18. Baba anafungua mikono yake 19. Wanawali kumi 20. Zakayo mbaya awa Zakayo mzuri 21. Hapa yuaja Yesu Mfalme 22. Yesu anawapenda rafiki zake 23. Msalaba 24. Yesu amefufuka kutoka kwa wafu! 25. Yesu anarejea nyumbani Mwongozo kwa wazazi

8 12 16 20 24 28 32 36 40 44 48 52 56 60 64 68 72 76 80 84 88 92 96 100 104 108


1. Mungu wangu ni Mku sana! (Mwanzo 1 & 2)

Mungu aliumba dunia yetu nzuri. Kwanza aliumba nuru. Aliumba jua liangaze mchana, na mwezi na nyota viangaze usiku. Pia aliumba bahari na nchi kavu. Kisha aliumba mimea na miti. Kila mahali kulikuwa na maua, miti ya matunda na mboga za kila aina.

8


Mungu wetu mkuu aliumba pia vitu vingine kwa ajili ya dunia hii nzuri ya ajabu kama vile samaki wanaoogelea na ndege wanaoimba kwa sauti tamu sana. Aliumba wanyama wa mwituni, wanyama wa kufugwa, wadudu wasio na madhara na wenye madhara. Kila kitu hutoka kwa Mungu.

9


Kisha Mungu alifanya kitu fulani maalumu sana… Aliwaumba watu wa kwanza. Mungu alimuita mwanaume Adamu, na mwanamke akamuita Eva. Bwana aliwapenda sana!

Njoo, tuombe pamoja: Bwana, wewe ni mkuu sana. Hakuna kitu chochote ambacho huwezi kufanya. Asante kwa kuumba dunia nzuri namna hii. Amen.

10


Mungu aliumba vitu vyote vizuri duniani.

Majina ya mwanaume na mwanamke wa kwanza yalikuwa ni yapi?

11


2. Daima msikilize Mungu! (Mwanzo 3)

Mungu aliwaweka Adamu na Eva mahali pazuri sana palipoitwa Bustani ya Edeni. Palikuwa ni mahali panapopendeza kuishi. Mungu aliwaambia, “Mnaweza kula kila kitu mtakachokikuta hapa. Lakini kuna mti mmoja maalumu; Hampaswi kula tunda litokanalo na mti huu. Mkila hakika mtakufa.” Siku moja mwovu shetani alijibadilisha na kuwa kama nyoka. Aliongea na Eva na kumwambia uongo wa kutisha. Nyoka alisema, “Unaweza kula tunda la mti huu maalumu. Hutakufa, kama Mungu alivyosema.”

12


13


Kisha Adamu na Eva wakala matunda kutoka kwenye ule mti. Mungu alihuzunika sana alipoona kwamba wamemuasi. Matokeo yake walilazimika kuondoka kwenye bustani ya Edeni. Mambo mabaya hutokea tunapoacha kumsikiliza Mungu. Bahati njema kwetu, Yesu alifanya kila kitu kuwa sawa tena wakati alipotoa maisha yake kwa ajili yetu.

Njoo, tuombe pamoja: Mpendwa Baba, tafadhali nisaidie niweze kukusikiliza wewe wakati wote. Amen.

14


Yesu alituosha dhambi zetu. Kila mara msikilize Mungu.

Adamu na Eva waliishi wapi?

15


3. Hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu! (Mwanzo 12, 13, 15, 17, 18 & 21)

Mungu alimwambia Abrahamu kwamba lazima aondoke katika nchi yake aende nchi nyingine. Abrahamu alimchukua Sara mke wake, pamoja na Loti mpwa wake. Kwa muda kitambo walikuwa na furaha, lakini baadaye wafanyakazi wa Loti na wafanyakazi wa Abrahamu wakaanza kugombana. Mara zote ni vibaya sana watu wanapopigana. Hivyo Abrahamu akamwambia Loti, “Lazima tuishi sehemu tofauti tofauti. Wewe chagua kwanza unataka kuishi wapi.” Loti alichagua eneo bora kabisa la ardhi kwa ajili yake.

16


17


Mungu alimwahidi Abrahamu kwamba atamtunza na kumpa familia kubwa sana; lakini Abrahamu na Sara hawakuwa na watoto. Walitaka sana watoto, lakini walikuwa wanazeeka. Je, Mungu alikuwa amesahau ahadi yake kwao? Siku moja watu watatu walikuja kumtembelea. Wakamwamwambia Abrahamu kwamba muda si mrefu Sara atakuwa na mtoto wa kiume. Sara aliposikia hili, alicheka. Mungu alitaka kujua kwa nini alikuwa anacheka. Je, alikuwa amesahau kwamba Mungu anaweza kufanya kitu chochote? Na muda si mrefu baadaye mtoto wa kiume alizaliwa nyumbani kwa Abrahamu na Sara. Walimuita jina lake Isaki.

Baba na Mama wa Isaki waliitwa nani?

18


Njoo, tuombe pamoja: Asante Bwana, kwamba unanijali na kwamba kwako hakuna jambo lisilowezekana. Amen.

Mungu anaweza kufanya mengi sana kuliko watu wanavyoweza! Hakuna lisilowezekana kwake.

19


4.Mungu amfanya punda aongee! (Hesabu 22)

Mfalme Balaki aliamua kumpa Balaamu fedha nyingi ili aseme mambo mabaya kwa watu wateule wa Mungu. Lakini Mungu aliamua kumzuia Balaamu. Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa njiani kuelekea kwa mfalme Balaki. Ghafla malaika wa Bwana akamtokea njiani. Alikuwa ameshika upanga.

20


Ni punda peke yake aliyeweza kumwona yule malaika. Balaamu hakuweza kumwona kabisa. Mara tatu, yule punda aligeuka njiani ili kumkwepa yule malaika. Kila mara alipofanya hivyo Balaamu alimpiga yule punda.

21


Kwa nini unanipiga?

Je, huwa mara zote ninaasi amri yako?

Kwa sababu unanikasirisha!

Hapana!

Jina la mtu ambaye punda wake aliongea aliitwa nani?

22


Kisha Bwana aliyafungua macho ya Balaamu, na ghafla akamwona yule malaika. Malaika akamwambia, “Kuanzia sasa na kuendelea utasema kile ambacho Mungu anakuambia kusema.” Na hicho hasa ndicho Balaamu alichokifanya.

Njoo, tuombe pamoja: Mpendwa Mungu, nisaidie nisiseme mambo ya ovyo na mabaya kuhusu watu wengine. Amen.

Yesu hapendi tunaposema mambo ya ovyo na mabaya kuhusu watu wengine. 23


5. Mungu husikia maombi yako (1 Samweli 1)

Elikana na mke wake Hana waliishi katika kijiji kidogo. Watu wa kile kijiji walimdhihaki Hana kwa sababu hakuwa na uwezo wa kupata watoto. Jambo hili lilimfanya akose kabisa furaha. Hana alimwomba Mungu hekaluni ili kwamba ampe mtoto. Alilia alipokuwa akiomba.

24


Eli, kuhani, alimwona akilia na kufikiri kwamba alikuwa amelewa. Alimkemea. Lakini Hana alipomsimulia kisa chake, Eli alitambua kwamba hakuwa amelewa. Hana alikuwa tu ana huzuni kubwa sana. Hivyo Eli akamwambia, “Mungu atakupa mtoto.” Na ilitokea kama ambavyo Eli alisema ingetokea.

25


Mtoto alizaliwa na walimwita jina lake Samweli. Mungu alikuwa mwema kwa Hana, kwa sababu baada ya Samweli alizaaa watoto wengine watano. Na hakuna mtu aliyemdhihaki tena.

Njoo, tuombe pamoja: Asante Yesu kwamba unasikia maombi yangu wakati wote. Amen.

26


Yesu hapendi tunapowadhihaki watu wengine.

Jina la yule mwanamke ambaye hakuweza kuwa na watoto ni nani?

27


6. Nena Bwana, ninasikiliza! (1 Samweli 3)

Mapema asubuhi moja kitu fulani maalumu kilitokea kwa Samweli. alikuwa akiishi na Eli ndani ya hekalu, lakini Eli alikuwa amelala. Sauti ikaita, “Samweli!” Samweli akajibu, “Ninakuja!” Kwa haraka akakimbia kwa Eli aliyekuwa katika usingizi, akamwambia, “Umeniita. Niko hapa.” Eli alitikisa kichwa chake akasema, “Mimi sijakuita.” Ilipotokea tena mara ya tatu, Eli alitambua kwamba Mungu ndiye alikuwa anamwita Samweli. Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Mara nyingine utakapoitwa, sema hivi, ‘Nena Bwana, ninasikiliza.’” Hivyo ndivyo hasa alivyofanya Samweli na Bwana akanena naye. 28


29


Alikumbuka hilo mpaka siku alipokufa. Kuanzia siku ile kila mtu alinena kuhusu Samweli, ambaye kila mara alifanya ambacho mungu alimwambia afanye.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, nisaidie kila mara nisikilize yale mambo unayoniambia katika Biblia. Amen.

30


Siku za leo Bwana huongea nasi kupitia Biblia.

Mungu aliongea na ……………………….?

31


7. Solomoni, Mfalme mwenye hekima (1 Wafalme 3)

Usiku mmoja Mfalme Solomoni aliota ndoto kwamba Mungu alimuuliza, “Je, ni kitu gani kimoja unakihitaji zaidi kutoka kwangu?” Solomoni akajibu, “Nisaidie niweze kufanya maamuzi kwa hekima.” Hivyo Mungu akamfanya Solomoni kuwa mwenye hekima kuliko watu wote duniani.

32


Siku moja wanawake wawili walikuja kumwona Mfalme Solomoni. Walimleta mtoto. Kila mwanamke alidai mtoto ni wa kwake. Mtoto wa mwanamke mmoja alikuwa amekufa usiku, kwa hiyo akawa ameiba mtoto wa mwanamke mwingine. Lakini ni mwanamke yupi alikuwa akisema ukweli? Ni yupi alikuwa ni mama yake halisi?

33


Solomoni akafanya mpango wa busara. Akasema, “Mpasue mtoto vipande viwili. Kisha kila mmoja wenu atapata nusu ya mtoto.” Mara hiyo hiyo mwanamke mmoja akasema, “Ndiyo mpasue nusu.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana, afadhali mpatie huyu mwanamke huyo mtoto. Tafadhali usimuuwe.” Solomoni akatambua mara moja kwamba yule mwanamke wa pili ndiye alikuwa mama halisi, kwa sababu alijali kweli kuhusu mtoto yule. Kwa hiyo akampatia huyo mwanamke yule mtoto. Kila mtu akanena kuhusu hekima yake kuu.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu nisaidie kila siku nikuletee furaha kwa kukusikiliza. Amen.

34


Kumbuka kuomba kila siku.

Ni nani alikuwa Mfalme mwenye hekima sana?

35


8. Mungu anatoa chakula na maji (1 Wafalme 17)

Eliya alikuwa ni mtu aliyeongea na Waisraeli kuhusu Mungu. Lakini Mfalme Ahabu na Waisraeli wengine walikataa kusikiliza ujumbe wa Mungu. Hivyo Eliya alimwambia Mfalme Ahabu kwamba mvua isingenyesha kwa muda mrefu sana, kwa sababu Ahabu hakumtumikia Mungu. Mfalme Ahabu aliamua Eliya auawe Mungu alimwambia Eliya aende kujificha katika pango karibu na kisima Pale, Eliya alikuwa na maji ya kunywa ya kutosha lakini hakuwa na chakula alisikia njaa sana. Hivyo Mungu aliwatuma kunguru wamletee mikate na nyama kwa kutumia midomo yao.

36


37


Walimletea Eliya chakula mara mbili kwa siku wakati wa asubuhi na wakati wa jioni. Eliya alijua kwamba Mungu angemtunza nyakati zote.

Njoo, tuombe pamoja: Mpendwa Baba, asante kwamba kila wakati unanitunza daima. Amen.

Daima sema asante kwa Yesu kwamba una kinywaji na chakula cha kutosha.

338 8


Mungu aliwatuma kunguru wamlishe nani?

39


9. Mungu ana nguvu kuliko Baali (1 Wafalme 18)

Eliya alikwenda kwa mfalme Ahabu na Yezebeli mke wake mkatili Aliwaambia “Ninakwenda kuwathibitishia kwamba Mungu ana nguvu kuliko mungu wenu Baali. Mwombeni Baali aunguze hili lundo la kuni. Nami nitamwomba Mungu afanye hivyo hivyo. Hakuna kilichotokea, Baali hakuweza kuunguza zile kuni. Hapakuwa kabisa na dalili ya uhai kutoka kwake. Kisha Eliya akamwaga maji katika lundo lake la kuni na kuomba. Mungu akashusha moto wa kuteketeza katika zile kuni.

40


41


Kila mtu aliona kwamba Mungu alikuwa mkuu na mwenye nguvu kuliko Baali. Hata hivyo Eliya hakuwa amemaliza. Akasema,“Mungu anaenda sasa kuleta mvua.” Anga lilikuwa angavu, isipokuwa wingu dogo lililokuwa na ukubwa wa mkono wa mtu. Mfalme Ahabu na watu wengine hawakuweza kuamini macho yao. Walipokuwa wakitazama anga likageuka kuwa giza kwa mawingu na mvua ikaanza kunyesha… na kunyesha… na kunyesha. Hakuna mwenye nguvu kama Mungu wetu.

Njoo, tuombe pamoja: Mungu Baba yetu asante kwamba wewe una nguvu sana na ni mwema sana kwetu. Amen. 442 2


Mungu ni mkuu na hakuna kitu ambacho hawezi kufanya.

Je, unafahamu majina ya mfalme na malkia?

43


10. Nehemia asaidia kuipendezesha tena Yerusalemu (Nehemia 1 - 7)

Nehemia alikuwa Mwisraeli. Alikuwa mnyweshaji katika ikulu ya mfalme wa Uajemi. Hii ilikuwa ni kazi muhimu, kwa sababu alikuwa anapaswa kuonja kila kitu kilichoandaliwa kwa ajili ya mfalme, kuhakikisha kwamba hakukuwa na sumu.

44


Baadhi ya Waisraeli waliokuwa wamerejea kutoka Yesusalemu walimweleza jinsi ambavyo jiji lilikuwa katika hali mbaya. Hata kuta za jiji zilikuwa zimeharibiwa. Mungu alitaka Nehemia arejee Yerusalemu kuwasaidia watu wake kuujenga upya tena huo mji. Nehemia alimpenda Mungu sana.

45


Alitambua kwamba alipaswa kumwomba mfalme wa Uajemi amruhusu arejee Yerusalemu mara hiyo hiyo. Alikuwa na wasiwasi kwamba mfalme angesemaje, hivyo alimwomba Mungu kwanza kabla ya kuzungumza na mfalme. Mungu alijibu maombi yake. Nehemia alirejea Yerusalemu. Huko waliujenga mji kwa kupendeza, na kuweka ahadi ya kumtii Mungu milele.

Njoo, tuombe pamoja: Mpendwa baba, nisaidie daima nikutii ili kwamba niweze pia kufanya mambo mazuri kwa ajili yako. Amen.

46


Hakuna kitu kinachotufanya tuwe na furaha zaidi kuliko umpenda Mungu.

Ni nani aliyejenga kuta za Yerusalemu?

47


11. Kwa msaada wa Mungu (Esta 1 - 10)

Esta alikuwa mwanamke mzuri sana wa sura. Alikuwa mzuri sana kiasi kwamba mfalme wa Uajemi alimwoa kuwa mkewe na akamfanya pia awe malkia. Siku moja mjomba wake aliyeitwa Mordekai, alikwenda kumtembelea. Mordekai akamwambia, “Wayahudi wote – ikiwa ni pamoja na wewe na mimi, tuko katika shida kubwa. Yule mtu mwovu Hamani, anataka kutuua sote. Alimwambia mfalme uwongo kuhusu sisi na sasa mfalme ameweka sheria inayosema kwamba katika siku moja fulani Wayahudi wote lazima wauawe.” Mordekai alipiga magoti mbele ya Esta na kusema, “Tafadhali Esta, tusaidie. Ni wewe tu unayeweza kutuokoa.”

48


Esta alimkaribisha mfalme na yule mwovu Hamani kwenye chakula cha jioni.

49


Alimwambia mfalme kuhusu njama za Hamani za kumuua yeye Esta na watu wake. Mfalme alimkasirikia sana Hamani. Aliweka sheria mpya ambayo iliwaokoa Wayahudi. Wayahudi walifurahi sana na wote wakapita mitaani wakicheza kwa furaha. Esta alikuwa mwanamke mjasiri aliyewaokoa watu wake kwa msaada wa Mungu.

Njoo, tuombe pamoja: Mpendwa Mungu, ninawasaidia watu wengine kwa sababu ninakupenda sana. Amen.

50


Mungu hutumia watu wa kawaida, kama wewe, mimi na Esta, ili kuwasaida wengine.

Taja mwanamke mzuri na jasiri alikuwa nani?

51


12. Danieli katika pango la simba (Danieli 6)

Danieli alikuwa Myahudi muhimu sana aliyeishi Uajemi. Kila mtu alijua jinsi alivyokuwa anampenda Mungu. Aliomba mara tatu kwa siku. Baadhi ya watu walimwonea wivu, hivyo walimwambia mfalme Dario aweke sheria mpya inayosema kwamba watu wangepaswa kuomba tu kwa mfalme, siyo kwa Mungu. Mtu yeyote ambaye angeivunja hiyo sheria angetupwa katika pango la simba. Danieli hakujali juu ya hiyo sheria mpya. Aliendelea kuomba kwa Mungu kama kawaida; asubuhi, mchana na jioni. Wale watu wenye wivu wakamwambia mfalme kwamba Danieli alikuwa anavunja sheria. 52


53


Hivyo Danieli akatupwa katika pango lililojaa simba. Mungu akawafunga midomo wale simba na Danieli alikuwa salama. Ndipo mfalme akatambua kwamba Mungu wa Danieli alikuwa Mungu wa pekee na wa kweli.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu, maisha yangu yako salama mikononi mwako. Amen.

54


Mungu anaweza kukusaidia wewe pia, kama vile alivyomsaidia Danieli katika pango la simba.

Ni nani alitupwa katika pango la simba?

55


13. Yona akataa kumtii Mungu (Yonah 2)

Mungu alimwambia Yona aende kwa watu wa Ninawi na awaambie waache kutenda dhambi. Yona hakutaka kumtii Mungu, hivyo akajaribu kumkimbia Mungu. Aliamua kupanda meli atoroke. Yona hakutambua kwamba hakuna mtu anayeweza kukimbia mbele za Mungu, kwa sababu Mungu anaona kila kitu.

56


Ghafla dhoruba ikaipiga ile meli ya Yona aliyokuwa amepanda. Kila mtu ndani ya ile meli aliogopa. Wakuu wa meli wakamtupa Yona baharini. Mungu akamtuma samaki mkubwa kumwokoa Yona na alimezwa na yule samaki. Akiwa ndani ya tumbo la samaki Yona alimwomba Mungu amsamehe kwa kutoroka.

57


Yule samaki alimtapika Yona kando / ufukweni mwa bahari. Kwa haraka Yona alikwenda Ninawi na kufanya kile Mungu alichomwambia. Aliwaambia watu waache kutenda mamabo mabaya. Watu walisema: “Bwana, tumekosa,” na Mungu aliwasamehe. Jambo hili lilimkasirisha Yona, kwa sababu hakuwapenda watu wa Ninawi. Mungu alisema anampenda kila mtu na hii ndiyo sababu aliwasamehe.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu, nisaidie kila wakati kusema nimekosa ninapofanya jambo lililo kinyume. Amen.

58


Sema umekosa kama umefanya jambo lililo baya. Yesu anampenda kila mtu, hata wewe pia. Ni nani alijaribu kukimbia kumtoroka Mungu?

59


14. Yesu amezaliwa (Luka 1 & 2)

Maria aliishi katika mji wa Nazareti. Alikuwa ameposwa na Yusufu. Siku moja alitembelewa na mgeni. Huyu hakumtembelea tu kama mtu mwingine yeyote; alikuwa ni Gabrieli, mmojawapo wa malaika wakuu wa Mungu. Alimwambia Maria kwamba atakwenda kumzaa mtoto, na mtoto huyo atakuwa Mwana wa Mungu. Maria akauliza, “Jambo hili litawezekanaje? Mimi sijaolewa bado.” Gabrieli akamwambia usiogope, kwa sababu hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu. Mtoto huyu atakuwa muujiza uliotumwa kutoka Mbinguni. 60


61


Maria akamjibu yule malaika, “Mwambie Mungu niko tayari kutii. Anaweza kunitumia kufanya jambo lolote analolitaka.” Malaika akaondoka, na maisha ya Maria kamwe hayakuwa tena kama yalivyokuwa. Baadaye Maria na Yusufu walioana. Ulikuwa ni wakati mkuu sana mtoto maalum kutoka mbinguni alipozaliwa katika Bethlehemu na Maria akambeba mikononi mwake. Yusufu akamwita yule mtoto jina lake Yesu. Naam, huyu mtoto Yesu angebadilisha ulimwengu wote.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana, ninakuabudu na kukusifu kwa sababu hakuna lisilowezekana kwako. Amen.

62


Jina Yesu linamaanisha: ‘Mungu huokoa’. Muulize Mama au Baba jina lako lina maana gani.

Yesu alizaliwa wapi?

63


15. Yesu anatembelea Hekalu (Luka 2)

Yesu aliendelea kukua vyema. Kila wakati aliwasikiliza wazazi wake. Siku moja Maria, Yusufu na Yesu walisafiri kwenda Yerusalemu. Walikwenda kwenye sherehe pamoja na Wayahudi wengine wote ili kumsifu Mungu kwa ukuu wake. Baada ya sherehe Yusufu na Maria wakiwa wameshika njia kurudi nyumbani waligundua jambo la kutisha: Yesu hakuwa pamoja nao!

64


Walimtafuta kila mahali, lakini Yesu hakuwa pamoja na watoto wengine ambao walikuwa sehemu ya kundi lile la wasafiri. Maria na Yusufu walipatwa na hofu kuu. Waliharakisha kurudi Yerusalemu kumtafuta Yesu. Walimtafuta kila mahali katika hilo jiji kubwa…

65


Hatimaye walimpata Yesu. Alikuwa ndani ya Hekalu. Walikuwa na furaha sana kumpata. Alikuwa anaongea na watu wenye hekima kuhusu Mungu. Wale watu wenye hekima walishangazwa kusikia jinsi Yesu alivyojua kuhusu Mungu kwa kiwango kikubwa. Wakiwa wamerejea Nazareti watu walijua kwamba Mungu alimpenda Yesu, nao pia walimpenda Yesu sana.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu, Nataka kuwa kama wewe. Amen.

66


Wazazi wako wanakutunza kama vile Yesu alivyotunzwa na wazazi wake.

Je, unayajua majina ya baba na mama yake Yesu?

67


16. Mikate mitano na samaki wawili (Yohana 6)

Watu wengi, wengi sana walitaka kumsikiliza Yesu akiongea kuhusu Mungu. Siku moja walimsikiliza Yesu hadi ukafika muda wa chakula na wakawa na njaa. Walikuwa wamesahahu kubeba vyakula.

68


Yesu aliwaambia rafiki zake wawape hao watu chakula, Andrea, mmojawapo wa rafiki zake, akamleta kijana mdogo kwa Yesu. Akasema, “Huyu kijana mdogo ana samaki wawili na mikate mitano, lakini hivi haviwezi kuulisha umati wote huu wa watu.”

69


Yesu akatabasamu na akachukua kile chakula kutoka kwa yule kijana mdogo. Kwanza kabisa Yesu akamshukuru baba yake kwa ajili ya kile chakula. Kisha akawagawia watu wote waliokuwa na njaa. Kulikuwa na chakula cha kutosha kwa kila mtu! Ulikuwa ni muujiza. Hata chakula kingine kilibaki. Wanafunzi wa Yesu wakakusanya chakula kilichobaki wakajaza vikapu kumi na viwili.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, najua ya kwamba unaweza kufanya kitu chochote. Amen.

770 0


Yesu alifanya miujiza ambayo hakuna mtu mwingine anaweza kufanya.

Unaweza kuhesabu vikapu vya chakula kilichobaki?

71


17. Hakuna mwingine kama Yesu (Luka 8)

Siku moja wakati Yesu akifundisha umati wa watu kuhusu Mungu, Yairo alijipenyeza katikati ya Watu mpaka mbele ya Yesu na kupiga magoti mbele yake. Akamwambia Yesu, “Binti yangu ni mgonjwa sana. Najua unaweza kumponya.” Yesu alikwenda pamoja na Yairo nyumbani kwake.

72


Walipokuwa bado wako njiani, watu walikuja wakikimbia kukutana nao na kuwaambia kwamba yule binti mdogo tayari ameshakufa. Yesu alimfariji Yairo. akamwambia, “Usiogope, amini tu.” Walipofika katika nyumba ya Yairo Yesu akawaambia watu waache kulia. Aliwaambia kwamba yule binti mdogo amelala tu, lakini walimcheka.

73


Yesu akaingia ndani ya nyumba. Akaushika mkono wa yule binti mdogo na kusema, “Amka!” Mara hiyo hiyo alijisikia vyema. Yesu aliwaambia familia yake wampatie huyo binti chakula. Kila mtu aliyemwona yule binti alijua kwamba hakuna mwingine aliye kama Yesu.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, kweli wewe ni wa ajabu. Nakupenda sana. Amen.

774 4


Hakuna mwingine aliye kama Yesu. Kumbuka Yesu anaweza kweli kukusaidia.

Je, Yesu alimponya binti wa nani?

75


18. Baba anafungua mikono yake (Luka 15)

Yesu alipenda kusimulia hadithi. Hii ni mojawapo ya hadithi zake bora kabisa... Palikuwepo na baba mmoja mzuri, ambaye aliwapenda sana watoto wake wawili. Siku moja yule mdogo aliamua kwamba anataka kuchukua pesa zake na kuondoka nyumbani.

76


kijana yule mdogo akasafiri kwenda nchi ya mbali, ambako alitapanya fedha zake. Fedha zake zilipokwisha, alitafuta kazi ya kulisha nguruwe. Alisikia njaa sana kiasi kwamba alitamani kula sehemu ya chakula cha nguruwe.

77


Mambo yaliendelea kuwa magumu kwake kiasi kwamba aliamua kurejea nyumbani kwa baba yake. Baba yake alikuwa anatarajia iko siku atarudi. Alipomwona mtoto wake akija barabarani, alimkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu. Baba yake alikuwa na furaha sana kumwona tena kiasi kwamba alimpa nguo mpya na kuandaa sherehe kubwa kusherehekea kurudi kwake nyumbani.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu, asante kwa kusimulia hadithi nzuri namna hii, ili kwamba tujifunze jinsi ambavyo unatupenda sana. Amen.

78


Baba yetu wa Mbinguni anatupenda wakati wote.

Yesu alipenda kufanya nini?

79


19. Wanawali kumi (Mathayo 25)

Yesu alisimulia hadithi hii pia... Wanawali kumi wakiwa na taa zao za mafuta walikuwa wanamsubiri mgeni maalumu aweze kufika. Hawakujua huyo mgeni atakuwepo pale saa ngapi. Waliacha taa zao zinawaka muda wote, kwa sababu kulikuwa na giza. Ni huzuni, kwamba ni wasichana watano tu walikuwa na busara ya kutosha na kuleta mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. Muda si mrefu, wanawali wote wakawa wanaanza kupiga mihayo, na kusinzia. Ghafla mtu fulani akapiga kelele, “Huyu hapa, mgeni maalumu amewasili!” Kwa haraka wale wanawali watano werevu walijaza taa zao mafuta ya ziada na kuziwasha. Wanawali wengine watano walilazimika kukimbilia duka la karibu kununua mafuta zaidi. 80


81


Yule mgeni maalumu alifurahi sana kuwaona wanawali watano werevu na walifanya sherehe ya kupendeza. Kulikuwa na vyakula na vinywaji vitamu. Wale wanawali wengine watano waliporejea, walikuwa wamechelewa sana kwenye ile sherehe. Walikosa shamrashamra zote.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu, ninataka kukuletea furaha na kuwa na wakati wa furaha na wewe siku moja huko mbinguni. Amen.

82


Daima fanya kila jema uwezalo kwa ajili ya Yesu, kwa sababu yeye daima hufanya lililo bora sana kwa ajili yako.

Ni wasichana wangapi waliokuwa na taa?

83


20. Zakayo mbaya awa Zakayo mzuri (Luka 19)

Zakayo alikuwa mtu tajiri sana aliyeishi katika mji wa Yeriko. Hakuna mtu yeyote aliyempenda kwa sababu alikuwa mkorofi kwa watu wengine. Zakayo alitamani sana kumwona Yesu, lakini alikuwa mfupi sana kuweza kumwona akiwa katika umati wa watu warefu.

84


Watu walimsukuma Zakayo mkorofi kwa kuwa hakuna mtu aliyependa kusimama karibu naye. Hivyo Zakayo akapanda juu ya mti uliokuwa karibu. Akiwa pale aliweza kumwona Yesu kwa uwazi sana.

85


Yesu akatazamana naye pale mtini uso kwa uso. Watu wote walishangaa wakati Yesu alipoanza kuongea naye. Na Zakayo alishangazwa wakati Yesu alipofika katika nyumba yake kula na kunywa naye. Kuanzia siku ile na kuendelea, ‘Zakayo mbaya’ akawa ‘Zakayo mzuri,’ na daima alikuwa tayari kumsaidia kila mtu.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, ninataka kuwasaidia watu wengine pia. Amen.

86


Watu wanaompenda Yesu hufurahia kuwasaidia watu wengine.

Taja ni mtu gani aliyepanda juu ya mti?

87


21. Hapa yuaja Yesu Mfalme (Mathayo 21)

Walipokaribia Yerusalemu, Yesu aliwaambia marafiki zake, “Nileteeni mwana punda.” Aliwaambia mahali ambapo wangempata yule punda na ni kitu gani wangemwambia yule mwenye punda. Marafiki wa Yesu walikwenda mahali pale punda alikokuwa. Walikuwa karibu kumchukua yule punda wakati mwenye punda alipowauliza, “Kwa nini mnamchukua punda wangu?” Wakamjibu. “Yesu ana haja naye.” Yule mtu aliposikia vile, alitosheka. Aliwapa huyo punda bila kusita.

88


89


Yesu alipanda yule punda kwenda mjini Yerusalemu. Umati wa watu ulijipanga barabarani. Walipepea angani matawi ya mti wa mtende na kupaza sauti, “Bwana asifiwe. Hapa yuaja Mfalme!”

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, ninataka kukuimbia sifa kila siku. Amen.

90


Mwambie kila mtu kwamba Yesu ni mfalme wa maisha yako.

Je, ni mnyama gani ambaye Yesu alimpanda?

91


22. Yesu anawapenda rafiki zake (Yohana 13)

Yesu na marafiki zake walikuwa siku zote wakitembea katika barabara zenye vumbi wakiwa wamevalia kandambili zao. Walipokuwa wameketi mezani kwa ajili ya chakula, Yesu aligundua kwamba miguu ya rafiki zake ni michafu. Alivua joho lake na kujifunga taulo kiunoni mwake. Kisha akamimina maji katika beseni. Akaanza kuwanawisha miguu rafiki zake, na kuifuta kwa ile taulo aliyojifunga. Petro alikuwa ni mmojawapo wa rafiki zake wakubwa. Kwa kawaida, hakupenda Yesu, akiwa kiongozi wake, amnawishe miguu. Akasema, “Kamwe wewe hutaninawisha miguu yangu.”

92


93


Yesu akamjibu, “Kama sitakunawisha miguu, hutakuwa na ushirika nami.” Hivyo Petro akamruhusu Yesu amwoshe miguu yake. Yesu alifanya hili kuwaonyesha rafiki zake ni kwa kiasi gani alikuwa anawapenda sana na kuwajali.

Njoo, tuombe pamoja: Yesu, nisaidie kila mara kuwapenda marafiki zangu. Amen.

94


Kumbuka kufanya mambo mazuri kwa marafiki zako. Yesu alifanya nini kwa marafiki zake?

95


23. Msalaba (Mathayo 27)

Maadui wa Yesu walitaka kumuua. Walikwenda kwa Pontio Pilato, mtu aliyekuwa muhimu sana katika nchi. Walimwambia athibitishe Yesu kwamba ana makosa; lakini Pilato hakuweza kupata kosa lolote ambalo Yesu alikuwa ametenda. Pilato akaamua kuwauliza watu afanye nini. Walipomwona Yesu wakapiga kelele, “Msulibishe!” Maadui wa Yesu wakawa wamemwambia afanye hivyo. Pilato akawaambia wamsulibishe mahali palipoitwa Golgota. Hapo wakamtundika Yesu juu ya msalaba katikati ya wahalifu wawili.

96


97


Yesu alipokuwa anakaribia kukata roho, akamwomba Mungu awasamehe watu waliokuwa wakatili sana kwake. Yesu alikufa siku ya Ijumaa mchana, ambayo leo inajulikana kama Ijumaa Kuu, kwa sababu katika siku hiyo Yesu alifanya iwezekane kwa watu tena kuwa marafiki zake Mungu.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, asante kwamba ulikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu. Amen.

98


Yesu alikufa msalabani ili kwamba makosa yote tunayofanya – dhambi zetu – ziweze kusamehewa.

Je, unaweza kutaja sehemu ambako Yesu alisulibiwa ni wapi?

99


24. Yesu amefufuka kutoka kwa wafu! (Mathayo 28)

Yesu alizikwa siku ile ile ya Ijumaa katika pango lililokuwa mali ya rafiki yake Yusufu. Kila mtu alikuwa na huzuni. Alfajiri na mapema siku ya Jumapili kundi la wanawake walikwenda kaburini. Walikuwa wakiwaza ni kwa jinsi gani wataweza kuingia kaburini, kwa sababu jiwe kubwa lilikuwa tayari limevingirishwa katika mlango wa kaburi. Lakini walipofika pale walikuta tayari jiwe limekwisha ondolewa… na kwamba kaburi lilikuwa wazi! Malaika akawaambia kwamba Yesu amefufuka kutoka kwa wafu.

100


101


Walikuwa na furaha sana. Waliharakisha kurudi ili kuwaambia marafiki wengine wa Yesu hizi habari njema. Mwanamke mmoja, Maria Magdalena, alirudi tena katika lile kaburi lililokuwa wazi. “Maria.” alisikia mtu akiita jina lake. Saa ile ile akajua ni Yesu. Alikimbia kwenda kuwaambia wengine kwamba amemwona Yesu kwa macho yake mwenyewe.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, asante kwamba wewe U hai, na kwamba nitaishi nawe milele. Amen.

102


Yesu yu hai! Na kila mtu anayempenda ataishi naye milele, hata kama amekufa. Ni nani aliyemwona Yesu kwa macho yake mwenyewe?

103


25. Yesu anarejea nyumbani (Matendo 1)

Marafiki wa Yesu walikuwa na furaha sana kumwona amerudi. Walijua kwamba hakuna mtu mwenye nguvu kama alivyo Yesu. Yeye ni mwenye nguvu hata zaidi ya kifo. Siku moja Yesu aliwaambia marafiki zake kwamba anapaswa kurudi kwa baba yake huko mbinguni, kwa sababu kwa asili, huko ndiko nyumbani kwake hasa. Pia aliwaambia wasiwe na huzuni, kwa sababu siku moja wataungana naye huko! Yesu na marafiki zake walipanda juu ya kilele cha mlima.

104


105


Wingu likashuka na kuwafunika. Wakati wingu lilipoinuka, likambeba Yesu kwenda naye. Marafiki zake, wakiwa na mioyo ya huzuni, wakamwangalia akienda zake mbinguni. Ghafla wakawaona malaika wawili wamesimama pale. Wale malaika wakawaambia wale mitume (hili ni jina walilopewa wale marafiki maalum wa Yesu) kwamba Yesu angerudi siku moja. Walipaswa kwenda na kuuambia ulimwengu wote kwamba Yesu anampenda kila mtu.

Njoo, tuombe pamoja: Bwana Yesu, ninajua utarudi kunichukua kwenda mbinguni, kwa sababu Biblia inaniambia hivyo. Amen.

106


Ingawaje Yesu yuko mbinguni, tunajua kwamba bado angali anatutunza.

Wingu lilimchukua Yesu kumpeleka wapi?

107


Mwongozo kwa wazazi Alama za kitabu cha Watoto cha CMP. Alama ya silka

Kila mtoto ni wa kipekee - hata hivyo kuna baadhi ya tabia ambazo zinakuwa kwa wanadamu wote ambazo zinaweza kugawanywa katika silka nne. Baadhi ya watoto hustawi katika mazingira ambako kuna sheia madhubuti, utaratibu imara wa maisha unaofuatwa na majukumu (watoto wa taratibu/kanuni/desturi); wengine hufurahia kuishi kwa muda ule ule na kufurahia kufanya mambo (watoto wa vitendo); kisha wako wale ambao hupendelea kutatua matatizo kwa njia ya kuumba, hata kama itamaanisha kufanya tofauti na njia inayojulikana (watoto wa kuuliza) na mwisho kuna watoto ambao wanaishi kulingana na ndoto zao za kufikirika na vithaminisho vyao (watoto wa kufikiria na walio na ukaribu na watu). Vitabu vya CMP vimeandaliwa kwa njia ambayo itaendana na kuvuta kila aina ya silka ya mtoto. Kwa maelezo ziadi kuhusiana na hizi silka tembelea tovuti yetu www.christianmediapublishing.com

Alama ya Maendeleo

Vitabu vya CMP vinatilia maanani tofauti ya ngazi za maendeleo za watoto. Lengo letu ni kuwasaidia wazazi na walezi kuweza kuwasisimua watoto kiakili na kihisia ili kuhakikisha kunakuwa na ukuaji wa kiwango cha juu katika maeneo haya. Kwa maelezo zaidi tembelelea tovuti yetu ya CMP www.christianmediapublishing.com

Alama ya Imani

Kuumbika kwa imani kwa hakika ni kwa namna ya pekee kwa kila mtoto; hata hivyo kuna tabia za jumla ambazo zinakuwa kwa kila mtoto. Kuna njia kuu tatu ambazo kupitia hizo watoto hujenga imani: • Wazazi kuwasomea watoto Biblia mara kwa mara, kuwasimulia hadithi za Biblia na zile zenye msingi wa Kibiblia, kuomba pamoja na kufanya shughuli za kujenga imani pamoja na watoto wao (kama zile ambazo zinapatikana katika kitabu hiki). • Watoto kuuliza maswali – wazazi wanatakiwa kuyachukulia maswali haya kwa umakini na kuyajibu kulingana na kiwango cha uwelewa wa mtoto. • Watoto hufuata kielelezo cha wale wanaowalea.

Alama za kihisia za werevu

Huwa tunapata hisia mapema sana kabla hatujajifunza lugha kuweza kuelezea jinsi vile tunavyojisikia. Kwa hivyo ni muhimu kwamba watoto wafundishwe kuelezea kwa maneno jinsi wanavyojisikia. Tumia vielelezo au picha zinazoendana na kila hadithi na muulize mtoto wako anafikiri yule mnyama au mtu katika picha anajisikiaje. Hili litawasaidia kutambua hisia zao wenyewe na hata hisia za watu wengine. Hili linatoa fursa ya kujifunza ambako mtoto anaweza kujifunza kujieleza jinsi ambavyo anajisikia.

108


Alama za Kusomea

Dunia ya ajabu sana inakuwa imefunguliwa kwa mtoto wako anapokuwa ameanza kujifunza kusoma. Furahia kila muda wa hii safari ya kusisimua pamoja na mtoto wako. Waruhusu waketi mapajani mwako ambako wanaweza kukaa kwa starehe na kujisikia salama na amani. Fungua kitabu ukiwa umekishika ili kwamba nyote wawili muweze kuona kurasa zake. Soma kwa ufasaha na kwa furaha. Kama ambavyo unajua, unaweza kusoma hadithi moja tena na tena. Unapokuwa unasoma onyesha kwa kidole ni mahali gani unaposoma. Hili litamsaidia mtoto wako kuanza kuona mahusiano yaliyoko baina ya herufi, sauti, maneno na maana zake. Mtoto wako anapojaribu kusoma, mtie moyo – hata kama anavyosoma inasikika kwako kama makorokocho.

Alama za ujuzi wa kusikiliza

Kusikiliza ni utalaamu muhimu wa kujifunza na kukua. Unaweza kusaidia kukuza huu utalaamu kwa mtoto wako kwa kumtia moyo kusikiliza kwa makini, na kuelewa kile anachokisikia. Waruhusu waangalie vielelezo vya picha na kisha watumie fikra zao kukusimulia tena hiyo hadithi kwa kutumia maneno yao wenyewe. Unaweza pia kuwatia moyo kufanya hili kwa njia ya kuuliza maswali yanayohusiana na hadithi hiyo. Njia nyingine pia ni kuondoa katika hadithi yale maneno ambayo mtoto anayafahamu vizuri na kumtaka ayajaze hayo maneno yanayokosekana.

Alama za msamiati (maneno magumu)

Tumia kila namna kujenga uelewa wa mtoto wako wa maneno magumu – ni zawadi ya maisha ambayo unampa mtoto wako. Anza kwa kutumia vitu mbalimbali vya kila siku na watu walioko katika vielelezo vya picha vitabuni. Onyesha ile picha, sema hilo neno lake. Jaribu kutumia hilo neno katika namna nyingine – kama kuna hema katika picha unayoiangalia basi unaweza kusema: huwa tunalala katika hema tunapokwenda katika kambi

Alama za kuunda semi

Tangu neno la mwanzo kabisa, nenda, jenga maneno ya mtoto wako – maneno ni matofali ya kujenga usemi. Unapoendelea taja vitu ambavyo vinakuzunguka, ukivionyesha. Hakikisha kwamba mtoto wako anaangalia mdomo wako, akipata hisia za midomo yako, koo lako unapokuwa unatamka hayo maneno. Kwa kadri mtoto wako anavyoendelea kukua, pole pole ongeza ugumu wa maneno yaliyotumiwa polepole ukiuvuta ufahamu wa mtoto wako. Kwa nguvu sana tia moyo jaribio la mtoto wako kuongea. Msaidie mtoto wako kutamka sauti na maneno katika hatua hii, usahihi siyo jambo la muhimu sana kama vile kujaribu.

Alama za ujuzi wa namba

Ni muhimu kwa mtoto wako kukua katika ujuzi wa namba. Chezeni michezo rahisi kama vile: “Kuna bata wangapi katika hii picha? Kama tukiongeza bata wengine wawili, sasa kutakuwa na bata wangapi?” Na ikiwa watatu wataruka (Tumia kidole chako kufafanua hili). watabaki wangapi? Pia watoto wanahitaji kutambua maumbo ya tarakimu. Kata maumbo makubwa ya namba kutoka kwenye boksi – waache watoto wako wacheze nazo – zipange hizo namba katika mtiririko ukianzia namba moja hadi kumi.

109


Biblia ya

-H

adithi

ina Maomb

© Haki zote zimehifadhiwa Christian Media Publishing, P.O. Box 3228, Matieland Post Office, Stellenbosch, 7602, South Africa www.christianmediapublishing.com Mtunzi: Ewald van Rensburg Vielelezo/picha: Lilani Brits Kusanifu na Kupanga kurasa: Lilani Brits Publishing Project Management: Noeline N Neumann Namba ya usajili 2010/008573/07 Hakuna sehemu ya chapisho hili linaloweza kutolea tena kwa njia yoyote – ya kieletroniki au vinginevyo vyote – bila ruhusa ya awali ya maandishi kutoka kwa mtoaji. Toleo la kwanza, Chapisho la kwanza 2014 ISBN 978-0-109205-92-4



Biblia hii inayovutia yenye vielelezo vya rangi iitwayo Yeskids imeandaliwa maalumu kwa watoto wa Yeskids! Kila hadithi imefuatiliwa na maombi kumsaidia mtoto aunganishwe na Mungu; kithaminisho cha Kikristo na mchezo wa kubahatisha ambao unakazia hiyo hadithi. Kitabu hiki kitawasaidia watoto wawe Yeskids. Mtoto wa Yeskids husema Ndiyo kuu! Katika kumfuata Yesu na katika kuishi maisha mema na ya furaha.

Mwongozo kwa wazazi: YesKids kimeandaliwa kwa kuzingatia hatua za kukua za mtoto wako na silka yake ya kipekee. Kinasaidia katika kujenga imani, maneno ya kuongea, na hata ujuzi wa kusoma na maendeleo ya kihisia. Kwa maelezo kamili ya alama fungua ukurasa wa 108 hadi 109.

Hatua za maendeleo

Silka za kipekee

Kujenga imani

Msamiati

Usemi

Ujuzi wa kusoma

Ujuzi wa kusikiliza

Mapendekezo namna ya kufurahia kitabu hiki na mtoto wako: • Someni hadithi ya Biblia, • Ongeeni juu ya hadithi na Vithaminisho vya Kikristo wewe pamoja na mtoto wako, • Chezeni mchezo wa kubahatisha na • Tamkeni maombi kwa pamoja.

Kwa kadri wewe na mtoto wako mnavyokuwa karibu na Mungu, ndivyo hivyo mtakuwa karibu kila mmoja kwa mwenzake.

The YesKids Bible – Stories and Prayers (kiSwahili)

ISBN: 978-0-10920-592-4

www.christianmediapublishing.com


Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.